Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Utekelezaji wa mkakati wa Matokeo Makubwa Sasa katika
Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) umeelezwa kuwa unakwenda vizuri.
Kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa hivi karibuni
inayoelezea utekelezwaji wa mkakati huo, pamekuwa na maendeleo makubwa na
kuongezeka kwa ufanisi katika bandari ya Dar es Salaam kulinganisha na kipindi
cha kabla ya mwezi wa saba mwaka jana.
Ripoti hiyo iliyotolewa na TPA inahusisha kipindi cha
kati ya Julai 2013 na Machi 2014.
Pamoja na mambo mengine, mkakati wa Matokeo Makubwa
Sasa unalenga kubadilisha bandari za Tanzania na hasa ile ya Dar es Salaam kuwa
kitovu kikuu cha uchumi Tanzania na kuwa shindani katika ukanda huu wa Afrika.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, pamekuwa na ongezeko la
mizigo katika bandari hiyo katika kipindi hicho kufikia tani milioni 10.95, hii
ikiwa ni mafanikio kwa asilimia 84.2 kabla ya kufikia lengo la tani milioni 13
kwa kipindi cha mwaka 2013/2014.
Muda wa meli kukaa bandarini kwa mwezi Machi 2014
ilikuwa siku 6.1 kwa meli, mafanikio ya asilimia 82.0 kabla ya kufikia lengo la
siku 5 kwa meli.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo muda wa kukaa kwa mizigo
bandarini kutoka nje kwa mwezi Machi 2014 ilikuwa siku 10.0 kwa kontena
kulinganisha na lengo la siku 7 kwa kontena.
“Hali hii imesababishwa na miundombinu mibovu ya reli
na kutegemea usafirishaji kwa njia ya barabara kwa kiwango kikubwa,” inasema
ripoti hiyo.
Uwezo wa kutoa magari bandarini umeongezeka kwa
asilimia 100.7 kwa mwezi Machi 2014, magari 604 yakitolewa kwa awamu.
Ripoti hiyo imeendelea kusema kuwa kwa mwezi Machi
2014 lengo la kutumia siku 3 kwa lori moja la mizigo kuwa limeondoka bandarini
limefikiwa kwa asilimia 81.1, kwani sasa lori moja linatumia siku 3.3.
Juhudi za kufanya bandari hiyo kufanya kazi kwa saa 24
kwa siku kwa siku saba za wiki ziko katika hatua za mwisho. Ripoti
ya makubaliano ya wadau wote wa serikali na sekta binafsi iliyofikiwa mwezi
Februari mwaka huu itajadiliwa hivi karibuni tayari kwa utekelezaji.
Ikiongelea kuhusu mfumo wa “Single Window Port Community System” unaolenga
kurahisisha kazi za nyaraka bandarini hapo, ripoti hiyo inasema tayari mfumo
huo umeshaanza kutumika tangu tarehe 25 mwezi uliopita.
Mfumo wa Terminal
operations system umeboreshwa ili
kuondokana na changamoto zilizokuwepo hapo mwanzo. Pia bandari kavu
mpya zimeanza kutumia mfumo huu.
Mifumo mbalimbali ya kisasa imeanzishwa katika juhudi
za kuongeza ufanisi bandarini hapo.
Mifumo hiyo ni pamoja na Harbour
view system; Cargo Operations System; Container operations system; Motor
vehicle operations system; Export receiving and loading operations system; Gate
operations system na Billing System.
Mwisho
No comments:
Post a Comment