Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe (wa pili kushoto)
akimueleza jambo Waziri wa Uchukuzi wa Jimbo la Katanga, Bw. Kahozi Sumba
wakati wa uzinduzi wa ofisi ndogo ya mawasiliano ya Mamlaka ya Bandari Tanzania
(TPA) mjini Lubumbashi katika jimbo hilo hivi karibuni. Wengine katika picha ni Mwenyekiti wa Kamati
ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Bw. Peter Serukamba (kushoto) na Kaimu
Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Eng. Madeni Kipande (kulia).
Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe (wa pili kushoto)
na Waziri wa Uchukuzi wa Jimbo la Katanga, Bw. Kahozi Sumba wakifuatilia jambo
wakati wa uzinduzi wa ofisi ofisi ndogo ya mawasiliano ya Mamlaka ya Bandari
Tanzania (TPA) mjini Lubumbashi katika jimbo hilo hivi karibuni. Wengine katika picha ni Mwenyekiti wa Kamati
ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Bw. Peter Serukamba (kushoto) na Kaimu
Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Eng. Madeni Kipande (kulia).
Sehemu ya wafanyabiashara wa DRC Congo waliohudhuria uzinduzi
wa ofisi ndogo ya mawasiliano ya Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) mjini
Lubumbashi, jimbo la Katanga hivi karibuni.
Uzinduzi huo ulifanywa na Waziri Harrison Mwakyembe kusaidia
wafanyabiashara wa nchi hiyo wanaotumia bandari ya Dar es Salaam.
Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe (katikati)
akisaini kitabu cha wageni katika ofisi mpya ndogo ya mawasiliano ya Mamlaka ya
Bandari Tanzania (TPA) mjini Lubumbashi, jimbo la Katanga hivi karibuni. Wanaoshuhudia ni Waziri wa Uchukuzi wa Jimbo
la Katanga, Bw. Kahozi Sumba (kushoto) na mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge
ya Miundombinu, Bi. Zarina Madabida (kulia).
Na Mwandishi wetu, Lubumbashi
Wafanyabiashara wa Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo (DRC)
wamesema wana matumaini makubwa na hatua ya Tanzania kufungua ofisi ndogo ya
mawasiliano ya Mamlaka ya Bandari (TPA) mjini Lubumbashi, jimbo la Katanga
nchini humo.
Wakiongea kwa niaba ya wenzao baada ya kuzinduliwa kwa ofisi
hiyo hivi karibuni, wafanyabiashara hao wanaopitisha mizigo yao katika bandari
ya Dar es Salaam, wamesema kuanzishwa kwa ofisi hiyo kumekuja wakati muafaka na
kuwa itawarahisishia biashara yao.
Sasa wafanyabiashara hao wataweza kufanya malipo ya bandari
wakiwa Lubumbashi na kuepuka hatari ya kusafiri na kiwango kikubwa cha pesa na
kuibiwa.
Mmoja wa wafanyabishara hao, Bw. Mubanzo Fils anayeendesha
kampuni ya ETS Mubanzo alisema jumuiya ya wafanyabiashara Lubumbashi imefurahia
sana kupata ofisi hiyo wanayotarajia kurahisisha kazi zao na kukuza biashara
baina ya nchi hizo mbili.
“Tuna furaha kubwa sana kwa hatua hii muhimu,” alisema.
Inatarajiwa kwamba tatizo lililokuwa linawakabili
wafanyabiashara hao la kukabiliana na wakala wa kupakia na kupakua mizigo wasio
waaminifu, sasa litakuwa historia kwa kuwa ofisi ya Lubumbashi itakuwa na
orodha ya wakala wanaokubalika na waaminifu.
Pia mienendo ya taarifa za mizigo itafanyika mjini humo na
hivyo kuharakisha taratibu za mizigo bandarini hapo.
Kwa upande wake, Bw. Lumbu Useni wa kampuni ya Luwang SPRL
alitoa wito kwa wafanyakazi kwenye ofisi hiyo ili kutimiza lengo lilikusudiwa.
“Wafanye kazi kwa bidii na akili zao zote ili lengo
lililokusudiwa na nchi hizi lifikiwe na sisi tuweze kufaidika,” alifafanua.
Mizigo ya DRC inayopita katika bandari ya Dar es Salaam
imekuwa ikiongezeka kwa asilimia takribani 24 kwa mwaka tangu mwaka 2004
ikiongezeka toka tani 155,611 hadi tani 1,117,249 mwaka 2013.
Nchi hiyo ni ya pili kwa kupitisha mizigo mingi katika
bandari ya Dar es Salaam. kwa mujibu wa
takwimu zilizopo, mizigo ya DRC inachukua asilimia 25 ya mizigo yote ya nchi
jirani inayopita katika bandari hiyo.
Mfanyabiashara mwingine, Bw. Mohamed Hassan Hammy, Mkurugenzi
Mtendaji wa kampuni ya Drill Tek ya mjini humo alisema Kongo ni soko kubwa
hivyo Tanzania imefanya busara kubwa kufungua ofisi hiyo.
Bw. Hammy ambaye ni mtanzania alisema pamoja na kwamba
kufungua ofisi hiyo ya TPA ni hatua kubwa, jumuiya ya wafanyabiashara mjini
hapo wanaomba serikali kufungua ofisi ndogo ya ubalozi wa Tanzania Lubumbashi ili
kuwasaidia katika mambo yao mbalimbali.
“Tunaipongeza serikali kufungua ofisi hii ya TPA lakini pia
tunaiomba ifungue ubalozi mdogo hapa Lubumbashi ili kutusaidia sisi watanzania
tunaoishi hapa,” alisema, na kuongeza kuwa kwa sasa wanalazimika kusafiri
umbali wa kilometa 2,000 hadi mjini Kinshasa wanapohitaji huduma za ubalozi wa
Tanzania.
“Kinshasa ni mbali sana na ni gharama kubwa,” alifafanua.
Awali, Waziri ya Uchukuzi wa jimbo la Katanga, Bw. Kahozi
Sumba alisema ufunguzi wa ofisi hiyo sio tu utarahisisha na kuleta ufanisi
katika kusafirisha mizigo ya wafanyabiashara wa Kongo wanaotumia bandari ya Dar
es Salaam, bali pia utasaidia kuboresha maisha yao.
“Kurahisisha biashara ina maana ya kupata maendeleo na
kuboresha maisha yetu, tunaishukuru sana serikali ya Tanzania kwa uamuzi huu,”
alisema baada uzinduzi huo uliofanywa na Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe.
Aliihimiza jumuiya ya wafanyabiashara wa nchi hiyo
kuthibitisha kuwa kweli walikuwa wanaihitaji ofisi hiyo kwa kuitumia kutatua
matatizo yao.
“Thibitisheni kwa vitendo kuwa kweli mlikuwa mnaihitaji ofisi
hii,” aliwaambia baadhi ya wafanyabiashara waliokuwa katika tukio hilo la
uzinduzi.
Mwisho
No comments:
Post a Comment