Monday, May 5, 2014

DRC yaisifu Tanzania kwa kufungua ofisi ya TPA Lubumbashi

Na Mwandishi wetu, Lubumbashi

Serikali ya Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo (DRC) imesema hatua ya Tanzania kufungua ofisi ndogo ya mawasiliano ya Mamlaka ya Bandari (TPA) ni ya kizalendo na inayothibitisha uhusiano mzuri uliopo baina ya nchi hizo.

Akiongea na waandishi wa habari hivi karibuni baada ya uzinduzi wa ofisi hiyo mjini Lubumbashi, jimbo la Katanga, Waziri ya Uchukuzi wa jimbo hilo, Bw. Kahozi Sumba alisema ufunguzi wa ofisi hiyo sio tu utarahisisha na kuleta ufanisi katika kusafirisha mizigo ya wafanyabiashara wa Kongo wanaotumia bandari ya Dar es Salaam, bali pia utasaidia kuboresha maisha yao.

“Kurahisisha biashara ina maana ya kupata maendeleo na kuboresha maisha yetu, tunaishukuru sana serikali ya Tanzania kwa uamuzi huu,” alisema baada uzinduzi huo uliofanywa na Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe.

Waziri Sumba alisema kuwa sasa serikali inatarajia kuwa wafanyabiashara wa Kongo hawatakumbana tena na changamoto walizokuwa wanakabiliana nazo awali katika biashara zao kati ya Kongo na Tanzania kupitia bandari ya Dar es Salaam.

Aliihimiza jumuia ya wafanyabiashara wa nchi hiyo kuthibitisha kuwa kweli walikuwa wanaihitaji ofisi hiyo kwa kuitumia kutatua matatizo yao.

“Thibitisheni kwa vitendo kuwa kweli mlikuwa mnaihitaji ofisi hii,” aliwaambia baadhi ya wafanyabiashara waliokuwa katika tukio hilo la uzinduzi.   
Awali, akiongea kwa niaba ya Gavana wa jimbo la Katanga, Bw. Moise Katumbi; Naibu Gavana wa jimbo hilo, Bw. Yav Guilbert alimmwagia sifa Waziri Mwakyembe akisema waziri huyo amethibitisha kuwa ni mtu wa vitendo.

Katika ziara yake mwezi Machi mwaka huu mjini Lubumbashi, Waziri Mwakyembe aliahidi kuwa ofisi hiyo ingekuwa tayari mwishoni mwa mwezi Aprili, jambo ambalo limetekelezwa kwa wakati.

“Waziri Mwakyembe si aina ya wanasiasa wanaotoa ahadi za uongo na ameonyesha kuwa Tanzania inaweza kuileta Afrika pamoja na kupata maendeleo,” alisema.

Awali, Dk. Mwakyembe alisema kuwa ofisi hiyo mpya itasaidia wafanyabiashara wa DRC kumaliza matatizo yao Lubumbashi badala ya kusafiri hadi Dar es Salaam.

“Wataweza kufanya malipo ya bandari wakiwa Lubumbashi na kuepuka hatari ya kusafiri na kiwango kikubwa cha pesa na kuibiwa,” alisema Waziri Mwakyembe.

Alisema tatizo lililokuwa linawakabili wafanyabiashara hao la kukabiliana na wakala wa kupakia na kupakua mizigo wasio waaminifu, sasa litakuwa historia kwa kuwa ofisi ya Lubumbashi itakuwa na orodha ya wakala wanaokubalika na waaminifu.

Pia mienendo ya taarifa za mizigo itafanyika mjini humo na hivyo kuharakisha taratibu za mizigo bandarini hapo.

Waziri Mwakyembe alisafiri kwa barabara tokea Dar es Salaam hadi Lubumbashi kupitia Zambia kwa barabara zaidi ya kilometa 2000 kuangalia na kupata taarifa za changamoto wanazokumbana nazo wafanyabiashara wa DRC kuanzia bandarini Dar es Salaam hadi njiani wanaposafiri.

Ofisi ya Lubumbashi inalenga kuondokana na changamoto mbalimbali zinazowakumba wafanyabishara hao zikiwemo ucheleweshaji, wizi, vikwazo visivyohusiana na kodi na wakala wa kupakia na kupakua mizigo wasio waaminifu.

“Juhudi zinaendelea kuhakikisha kuwa vikwazo na urasimu wote unaowakabili wafanyabiashara wa DRC unakwisha,” alifafanua Waziri.
Mizigo ya DRC imekuwa ikiongezeka kwa asilimia takribani 24 kwa mwaka tangu mwaka 2004 ikiongezeka toka tani 155,611 hadi tani 1,117,249 mwaka 2013.

Nchi ya DRC ni ya pili kwa kupitisha mizigo mingi katika bandari ya Dar es Salaam.  kwa mujibu wa takwimu zilizopo, mizigo ya DRC inachukua asilimia 25 ya mizigo yote ya nchi jirani inayopita katika bandari hiyo.

Pamoja na maafisa wengine, ujumbe wa Tanzania Lubumbashi ulijumuisha Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Bw. Peter Serukamba, mjumbe wa kamati hiyo, Bi. Zarina Madabida, maafisa waandamizi toka TPA, Mamlaka ya Usafiri wa nchi kavu na Majini (SUMATRA), Tanzania Railways Limited (TRL), TAZARA na wengine.

Mwisho


No comments: