Monday, May 5, 2014

Ole Naiko apigia debe Mfuko wa mitaji wa wafanyabiashara(Mkoba)

Mlezi wa  Asasi ya Diana Women Empowerment Organization ambaye pia Balozi wa Heshima wa Botswana nchini Tanzania, Bw. Emanuel Ole Naiko kati akifungua semina ya mafunzo ya wajasiriamali ambao ni wanachama wa asasi hiyo jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki. Kulia ni Mwenyekiti wa taifa wa asasi hiyo, Bi. Farida Khakoo na kushoto ni Katibu wa Taifa wa asasi hiyo, Bi. Joyce Singano.
Mlezi wa  Asasi ya Diana Women Empowerment Organizationambaye pia Balozi wa Heshima wa Botswana nchini Tanzania, Bw. Emanuel Ole Naiko kulia akiangalia kazi za mikono zinazotengenezwa na wajasiriamali ambao ni wanachama wa asasi hiyo  na kushoto ni Mwenyekti wa asasi hiyo taifa, Bi. Farida Khakoo.
Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Mfuko wa Mitaji ya Wafanyabiashara (Mkoba Private Equity Fund) uliozinduliwa na Rais Jakaya Kikwete  hivi karibuni umeelezwa kuwa ni kimbilio kubwa kwa wafanyabiashara wadogo na wa kati katika kupata mitaji ya kukuza biashara zao.

Mlezi wa Asasi ya Diana Women Empowerment Organization ambaye pia ni Balozi wa Heshima wa nchi ya Botswana hapa Tanzania, Mhandisi Emmanuel Ole Naiko ameuelezea mfuko huo kama kimbilio la wajasiriamali.

“Uzinduzi wa mfuko huo umekuja wakati mwafaka kwa vile Tanzania tuna tatizo kwa wajasiriamali wadogo na wakati kupata mitaji ya kuendeleza na kukuza shughuli zao za kibiashara,” Bw. Ole Naiko aliyasema hayo mwishoni mwa wiki  jijini Dar es Salaam wakati akifungua  semina ya siku moja ya wajasirimali wa asasi hiyo.

Alisema serikali kupitia Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC),  imejitahidi kuweka mifumo mizuri ya sheria kwa ajili ya wawekezaji wa ndani na nje lakini tatizo lililpo ni namna ya kupata mitaji kwa vile benki zina masharti magumu ya kupata mikopo.

“Kwa  kweli uzinduzi wa mfuko huo utasaidia sana kuchochea shughuli za biashara na ujasiriamali hapa nchini kwa vile kutakuwa na sehemu ya kupata mitaji,” alisema na kuongeza kuwa ni vyema wajasiriamali wakachangamkia fursa za kuwepo kwa mfuko huo.

Bw. Ole Naiko  aliwaasa pia  waanasemina hao kuzingatia mafunzo ya ujasiriamali na kwamba elimu, mbinu na maarifa  wanayoyapata wakayatumie  kwa vitendo ili kuzidi kuendeleza kibiashara.

“Mafanikio katika biashara yanaanza kwa mtu mwenyewe na hakuna mtu anayeweza kuja kuwaendeleza katika biashara zenu bila  wenyewe kujitambua na kujiongezea maarifa”aliongeza kusema.

Aliwaasa wajasiriamali hao kuzitumie fursa zinazojitokeza za kupata mikopo kwa ajili ya kukuza biashara kwa faida yao na taifa kwa ujumla kwani mchango wa wajasiriliamali ni mkubwa sana.
 Mwenyekiti wa Taifa wa Asasi hiyo, Bi. Farida Khakoo alisema semina hiyo ilishirikisha wanasemina 40 ambao ni wajasiriamali na wanachama wa asasi hiyo.

“Asasi yetu inalea watoto yatima, walemavu na wajane na ina wanachama ambao ni wajasiriamali,”alisema.
Alisema semina hiyo inalenga kuwafundisha wajasiriamali hao nanma ya kutunza kumbukumbu za hesabu za biashara zao katika vitabu ili waweze kuendesha vema biashara.

Naye mwanachma na mjasirimali wa asasi hiyo,Bi. Constance Chandende alisema semina hiyo itamwezesha kupata ujuzi zaidi wa kuendesha shughuli zake za ujasiriamali na kufikia malengo.

“Mimi biashara yangu ni ya kusindika matunda yakiwemo ya pilipili mbuzi, michaichai, maembe na mbilimbi,”alisema.

Alisema wanawake wengine nchini wasikae bila kazi bali yajiingize katika biashara mabalimbali ili waweze kuwa na mchango katika familia.

Mwisho.


No comments: