Tuesday, May 13, 2014

Bank of Africa Tanzania yaanza kutoa mikopo sekta ya afya

Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Bank of Africa Tanzania imeanza kutoa mikopo yenye riba nafuu kwa sekta ya afya ili kuwezesha zahanati, vituo vya afya na hospitali kutoa huduma bora kwa wananchi.

Meneja Mwandamizi wa Masoko wa benki hiyo, Bw. Solomoni Haule aliwaambia waandishi wa habari mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam kuwa mikopo hiyo itawezesha sekta hiyo kutoa huduma boara kwa jamii.

“Benki imeanza kutoa mikopo kwa sekta ya afya ili kuwezesha sekta hiyo muhimu kuweza kutoa huduma bora na hivyo kuleta maendeleo,” alisema.
Alisema mikopo hiyo iliyoanza kutolewa April mwaka huu ni ya riba nafuu na inatolewa kwa  muda mfupi na muda mrefu unaokwenda hadi miaka minne.
Huduma hiyo ya mikopo inaitwa ‘Tiba Finance.’

Alisema benki inaamini kuwa changamoto kubwa zinazokabili sekta hiyo kama vitendea kazi, mashine za kisasa, kujenga na kukarabati majengo, na dawa za kutosha zinaweza kupungua na hatimae kuisha kabisa kutokana na huduma ya mikopo hiyo.

“Kupitia mikopo hii tunaamini wataweza kumaliza au kupunguza kwa kiasi kikubwa changamoto hizi,”alisema.

Alisema katika kufanikisha azma hiyo benki inashirikiana na asasi ya Medical Credit Fund kuzijengea uwezo taasisi hizo ili ziweze kutoa huduma bora.
“Tumejipanga kwa kushirikiana na asasi hii kwenda katika kila taasisi itakayokopa kutoa elimu,”alisema.

Watafundisha matumizi namna ya kutumia vifaa vya kisasa vya kitabibu, mazingira ya kazi, utendaji, na kutengeneza mipango ya mahesabu ya kibiashara.

Alisema benki yao tayari ilishawapatia semina wafanyakazi wake tayari kutoa mikopo kwa sekta hiyo ya afya.

Bank of Africa ilianza huduma zake zaidi ya miaka 30 iliyopita huko Bamako, Mali.

Kwa hapa nchini, benki hii ina zaidi ya miaka saba ikihudumia makampuni makubwa pamoja na kada ya wajasiriamali wadogo na wa kati.

Kwa sasa ina matawi katika mikoa ya Dar es Salaam (yenye matawi kumi), na mengine katika mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Morogoro, Mtibwa, Mbeya, Tunduma, Mwanza, Kahama na sasa Mtwara.


Mwisho

No comments: