Friday, May 9, 2014

Benki ya Afrika Tanzania yapunguza riba kwa mikopo ya nyumba

Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam

Benki ya Afrika Tanzania imetoa ofa ya miezi sita ya pugunzo la riba ya mkopo ya nyumba kutoka asilimia 18 hadi kufikia asilimia 16 ili kuwawezesha wananchi wengi kumiliki nyumba.

Meneja Mwandamizi wa Masoko wa benki hiyo, Bw. Solomon Haule aliwaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana kuwa ofa ya punguzo hilo la riba linalenga kuwawezesha wanachi kuweza kumiliki nyumba.

“Ofa hii ilianza mwezi Mei mwaka huu na itadumu kwa muda wa miezi sita,” alisema.

Alisema punguzo hilo ni kubwa ukilinganisha na hali halisi, lakini benki imeamua kufanya hivyo kwa ajili ya kuwawezesha watanzania wengi kumiliki nyumba za kuishi au biashara kwa kuwa maswala hayo ni ya msingi kwa ustawi wa jamii.

Licha ya punguzo hilo, benki imeongeza muda wa kulipa mkopo kutoka miaka 15 hadi miaka 20 ambayo inatoa fursa kwa watu wengi kuitumia.

Alihamasisha watu wengi hasa vijana kujitokeza na kuitumia fursa hiyo.

Alisema mtu anayestahili kupata mkopo ni yule mwenye mshahara au kipato cha Tshs 1.4 milioni kwa mwezi au watu wawili wanaoshirikiana kutaka kumiliki nyumba kama baba na mama ambao watakuwa na pato la pamoja la Tshs milioni 2 kwa mwezi. 

Akitoa mfano alisema mkopo huo utawawezesha wananchi kununua nyumba za bei rahisi zinazojengwa na mashirika hapa nchini yakiwemo Shirika la Taifa la Nyumba (HNC), Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) na Mfuko wa Mafao wa Watumishi wa Umma (PSPF).

“Siyo kwenye mashirika hayo tu bali hata ukiona nyumba inauzwa na mtu binafsi pia tumia fursa hii kumiliki nyumba,”alisema Bw. Solomon.

Akifafanua zaidi alisema ili kupata mkopo huo, mteja atatakiwa kuwa na asilimia 10 na benki itampatia mkopo wa asilimia 90 kwa nyumba mpya na asilimia 20 kwa nyumba iliyotumika.

Kwa mtu anayemiliki nyumba lakini anataka kupata fedha ya mtaji, benki itatathimini nyumba yake kisha itampatia mkopo wa asilimia 70 ya thamani ya nyumba yake.

Pia mteja anayemiliki nyumba na anataka kuwa na nyumba ya pili, pia benki itafanya tathimini ya nyumba yake na itampatia mkopo wa asilimia 70 na anayetaka kumalizia nyumba au kuiboresha atapata mkopo wa asilimia 40.

Bank of Africa Tanzania ilianza huduma zake zaidi ya miaka 30 iliyopita huko Bamako, Mali.

Kwa hapa nchini, benki hii ina zaidi ya miaka saba ikihudumia makampuni makubwa pamoja na kada ya wajasiriamali wadogo na wa kati.

Kwa sasa ina matawi katika mikoa ya Dar es Salaam (yenye matawi kumi), na mengine katika mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Morogoro, Mtibwa, Mbeya, Tunduma, Mwanza, Kahama na sasa Mtwara.


Mwisho

No comments: