Wednesday, May 21, 2014

Benki ya Afrika Tanzania yatoa msaada wa vitabu

Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Katika kuhakikisha inasaidia sekta ya elimu, Benki ya Afrika Tanzania imezindua programu ya kusaidia sekta hiyo vitabu katika shule za sekondari nchini.

Kwa kuanza, benki hiyo imetoa vitabu kwa shule ya sekondari Tandika ambayo imepatiwa vitabu vya sayansi na arts ili kuwawezesha wanafunzi wake kufanya vizuri kimasomo.

Meneja Mwandamizi wa Masoko na Mawasiliano wa benki hiyo, Bw.Solomon Haule alisema mara baada ya kukabidhi vitabu hivyo jana jijini Dar es Salaam kuwa benki yao imezindua programu hiyo ili kuwezesha wanafunzi kufanya vizuri kimasomo.

“Benki yetu imetenga sehemu ya faida yake katika mwaka huu wa fedha kwa ajili ya kusaidia sekta ya elimu ili kuunga mkono juhudi zinazofanywa na serikili katika sekta ya elimu,”alisema Bw. Haule.

Alisema benki yao inatambua kuwa serikali pekee haiwezi kufanya kila kitu na badala yake  wadau mbalimbali wanahitajika kushiriki katika kulijenga taifa hasa katika sekta ya elimu na nyingine.

“Baada ya kutoa msaada huu tutaendelea katika shule nyingine ili kuziwezesha shule  nyingi kuwa na vitabu vya kutosha,”alisema.

Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Bw.Hussein Mpugus alisema vitabu hivyo vitasaidia wanafunzi kufanya vizuri katika masomo yao.

“Tunashukuru kwa dhati kupata vitabu hivi...ni msaada mkubwa,”alisema.
Alisema mahusiano hayo yaliyojengwa kati ya shule yake na benki yanapaswa kuzidi kuendelezwa kwa vile yanalenga kuboresha elimu inayotolewa shuleni hapo kwa mafufaa ya wanafunzi na taifa.

Aliihakikishia benki hiyo kuwa watavitumia vitabu hivyo kwa uangalifu ili hata wanafunzi wengine watakao kuja waweze kuvikuta na kuvitumia.

Naye Kaka Mkuu wa Shule hiyo, Bw. Hamza Msanga alisema shule yao ilikuwa na changamoto ya vitabu kwa wanafunzi na kuwa sasa imepatiwa majibu na benki hiyo.

“Tutahakikisha tunasoma kwa bidii...huu ndiyo msaada ambao wanafunzi tunastahili kupatiwa,” alisema.

Aliziomba taasisi nyingine kuiga mfano ulioonyeshwa na benki hiyo ili kuweza kuisaidia shule yao ambayo ina changamoto mbalimbali.

Bank of Africa Tanzania ilianza huduma zake zaidi ya miaka 30 iliyopita huko Bamako, Mali.

Kwa hapa nchini, benki hii ina zaidi ya miaka saba ikihudumia makampuni makubwa pamoja na kada ya wajasiriamali wadogo na wa kati.

Kwa sasa ina matawi katika mikoa ya Dar es Salaam (yenye matawi kumi), na mengine katika mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Morogoro, Mtibwa, Mbeya, Tunduma, Mwanza, Kahama na sasa Mtwara.


Mwisho.

No comments: