Wednesday, April 30, 2014

Maghembe asema tatizo la maji kuwa historia Karatu

Rais wa Jmahuri ya Muungano wa Tanzania DKT. Jakaya Mrisho Kikwete ( wa pili kulia) akisikiliza maelezo kutoka kwa mkurugenzi wa Mamlaka ya maji Mkoani Arusha ( AUWSA) mhandisi Ruth Koya wakati wa sherehe fupi za uzinduzi wa  hatua ya kwanza ya mradi wa upatikanaji wa maji safi na salama katika mji wa Karatu mkoani Arusha hivi karibuni, mwisho kulia ni Waziri wa maji Profesa Jumanne Maghembe, wengine katika picha ni mkuu wa mkoa wa Arusha Bw. Magesa Mulongo wa tatu kulia.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania DKT. Jakaya Mrisho Kikwete (kulia) akimtwisha ndoo ya maji Joan Israel, muda mfupi mara baada ya kuzindua hatua ya kwanza ya mradi wa upatikanaji wa maji safi na salama katika mji wa Karatu mkoani Arusha hivi karibuni, anaeshuhudia ni Waziri wa maji Profesa Jumanne Maghembe.
Rais wa Jmahuri ya Muungano wa Tanzania DKT. Jakaya Mrisho Kikwete (kulia) akifurahia jambo na Waziri wa maji Profesa Jumanne Maghembe mara baada ya kufungua maji wakati wa sherehe fupi za uzinduzi wa  hatua ya kwanza ya mradi wa upatikanaji wa maji safi na salama katika mji wa Karatu mkoani Arusha hivi karibuni, katikati ni Mkurugenzi wa Mamlaka ya maji mkani Arusha ( AUWSA)  mhandisi Ruth Koya.
Na Mwandishi Wetu, Karatu.
Hatua ya kwanza ya mradi wa upatikanaji wa maji katika mji wa Karatu jijini Arusha umefikia asilimia 34, huku shilingi milioni 310 zikihitajika kukamilisha hatua hatua hiyo, ambapo mradi mzima ukitarajia kugharimu sh.mil 620.7.

Waziri wa maji Profesa Jumanne Maghembe aliyasema hayo Wilayani Karatu, jijini Arusha wakati alipokuwa akizungumza na mwandishi wa gazeti hili juu ya mpango wa ukamilishaji wa miradi ya maji katika baadhi ya maeneo ya miji midogo na mikubwa hapa nchini.

“Fedha hizo kwa ajili ya kukamilisha awamu ya kwanza ya mradi huo, tutazitoa kabla ya mwaka huu wa fedha haujaisha ili kumaliza awamu hiyo,” alisema Waziri wa maji.

Alisema kuanzia mwaka wa fedha unaokuja 2014 – 2015 wizara itahakikisha kwamba mradi unapanuliwa kufikia upande wote wa magharibi  wa mji huo.

Aliongeza kuwa hadi kufikia mwakani mwezi wa 4 mji wa Karatu na maeneo ya jirani hakutakuwa na shida ya maji kama mwaka 2013.

“ Nawahakikishia wananchi wa Karatu kuwa ifikapo mwaka 2015 mwezi kama huu hawatakuwa na upungufu wa maji tena” aliongeza.

Mji huo wenye wakazi 42, 000 unahitaji takribani lita 4,000, 000 kwa siku ambapo kwa sasa upatikanaji wa maji ni lita 850, 000 ambazo hazitoshelezi mahitaji ya wananchi wa mji huo.

Alisema baada ya kuchimbwa kwa visima viwili katika mji huo kutapunguza adha hiyo kwa kiasi kikubwa kwa wananchi wa Karatu.

Alisema uendelezaji wa awamu ya pili ya mradi huo ni kuongeza uchimbaji wa visima pamoja na kujenga matenki kwa ajili ya kuhifadhia maji katika maeneo ya Karatu magharibi na eneo la G. lambo.
“Katika awamu hii ya pili zaidi ya shilingi mil.700 zitahitajika ili kufanikisha kukamilisha awamu hii,” alisema.

Baadhi ya wakazi wa mji wa Karatu wamesifu hatua hiyo ya serikali kupitia wizara ya maji kuwa wananchi wa Karatu sasa watakua wamekombolewa katika adha kubwa iliyokuwepo awali.

“Hii ni kama neema kwetu kwa kweli serikali imetujali sana ,” alisema Joseph Macha.

Aliongeza kuwa kwa muda mrefu wamekuwa katika tabu, wakina mama walikuwa wakifuata maji umbali mrefu, hivyo kuzorotesha shughuli nyingine za kimaendeleo.

Nae Joan Israel alisema wakina mama wa Karatu sasa watakuwa na nafuu ya kuamka asubuhi kutafuta maji, kwani kilichofanywa na wizara ni kitendo kinachoonyesha kuwa serikali inawajali wananchi wake.
“ mimi niseme tu kwamba, Mungu awabariki hawa viongozi wetu, Rais Kikwete pamoja na waziri wa maji Jumanne Maghembe wamefanya kazi kubwa kuwaokoa kina mama wa Karatu,” alisema.

Mwisho.


No comments: