Tuesday, April 22, 2014

TTCL yatoa mkono wa sikukuu ya Pasaka kwa vituo vya kulelea watoto yatima

Mkuu wa Biashara wa kampuni ya Mawasiliano Tanzania (TTCL), Kanda ya Dar es Salaam, Bw.Karim Bablia (kushoto) akimkabidhi msaada wa vyakula Katibu Mtendaji wa kituo cha watoto yatima cha Chakuwama Orphanage Centre, Bw. Hassan Hamis kwa ajili ya sherehe za sikuku ya Pasaka mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam.
Mkuu wa Biashara wa kampuni ya Mawasiliano Tanzania (TTCL), Kanda ya Dar es Salaam, Bw.Karim Bablia akiwakabidhi watoto Hassan Ameir (kulia) na Hashimu Shireni (katikati) kutoka Chakuwama Orphanage Centre msaada wa vyakula kwa ajili ya sherehe za sikuku ya Pasaka mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam.
Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam

Wakati wakristo wote kote duniani wanaposherekea sikukuu ya Pasaka, Kampuni ya Mawasiliano Tanzania (TTCL) imetumia fursa hiyo kutoa msaada wa vyakula kwa vituo vitatu vya watoto yatima

Akikabidhi msaada huo, Mkuu wa Biashara Mkoa wa Dar es Salaam wa kampuni hiyo,  Bw. Karim Bablia alisema msaada huo unalenga kuvisaidia vituo hivyo vya kulelea watoto yatima vya jijini Dar es Salaam ili nao waweze kusherehekea vyema sikukuu hiyo ya pasaka.

“Kampuni yetu imeamua kusherekea pamoja na watoto hawa ambao pia ni sehemu ya jamii yetu,”alisema Bw. Bablia.

Alivitaja vituo vilivyopatiwa msaada huo kuwa ni pamona na Hananasifu Orphanage cha Mkwajuni Kinondoni, Yatima Group Trust Fund cha Chamazi Mbagala na Chakuwama Orphanage Centre cha Sinza Mori.

Alisema msaada huo ni  pamoja na kilo 450 za mchele, maharage kilo 300, Unga kilo 750, katoni 100 za maji ya kunjwa, lita 120 za mfuta ya kupikia na sabuni katoni 15 ambapo vituo hivyo vyote vitagawiwa.

Alisema msaada huo ni sehemu ya ushirikiano mzuri kati ya TTCL na wateja wake hivyo kuwapatia watoto yatima ni sawa na kurudisha fadhila kwa wateja wao kutokana na ushirikiano wao.

“Tunatambua kuwa kulea na kutunza watoto yatima ni wito mkubwa kwa watu au vituo vilivyo jitolea kufanya hivyo,”alisema Bw. Bablia.

Mkurugenzi Msaidizi wa Yatima Group Trust Fund, Bw. Haruna Mtandika alisema kituo chao kina watoto 179 ambao wanasaidia kwa kulelewa na kupatiwa mahitaji mbalimbali ya kibinadamu.

“Tunaishukuru kampuni yetu ya TTCL kwa kutupatia msaada wa vyakula, hii itasaidia watoto wetu kusherekea vyema sikukuu hii ya Pasaka,” alisema.

Alisema kituo chao kimejitolea kulea watoto yatima ambao walikuwa wanaishi katika mazingira magumu sana ili waweze kupata huduma za msingi ili badaye waje kuwa watu wanaoweza kujitegemea.

Naye Katibu wa Mtendaji wa Chakuwama Orphanage Center, Bw. Hassan Hamis alisema anashukuru msaada huo kwa vile watoto wake nao watafurahia sikukuu ya Pasaka.

“Kituo chetu kina watoto 90 na kinajitahidi kadiri ya uwezo wake katika kulea watoto hao yatima lakini kinakabiliwa na changamoto mbalimbali,”alisema Bw. Hamis.

TTCL imekuwa na utaratibu wa kutoa misaada kama hii kwa muda mrefu sasa.


Mwisho

No comments: