Wednesday, April 2, 2014

Serikali yawahakikishia wananchi Ngudu maji ya uhakika

Waziri wa Maji Profesa Jumanne Maghembe ( kushoto) akicheza ngoma ya kabila la kisukuma aina ya Gumulo Dance na kijana Masunga Maganga wakati wa sherehe fupi za uwekaji jiwe la msingi kwa ajili ya mradi wa upanuzi wa mtandao wa maji ya ziwa Victoria kutoka katika kijiji cha Mhalo hadi katika  mji mdogo wa Ngudu, anaeshuhudia ni Mbunge wa Jimbo la Kwimba Mh. Shanif Mansoor, uwekaji huo wa jiwe la msingi ulifanyika hivi karibuni katika mji mdogo wa Ngudu Wilayani Kwimba Mkoani Mwanza.
Waziri wa Maji Profesa Jumanne Maghembe ( katikati ) akizungumza jambo na Mbunge wa Jimbo la Kwimba Mh. Shanif Mansoor wakati alipofanya ziara katika Wilaya ya Kwimba Mkoani Mwanza hivi karibuni na kuweka jiwe la msingi kwa ajili ya mradi wa upanuzi wa mtandao wa maji ya ziwa Victoria kutoka katika kijiji cha Mhalo hadi mji wa ngudu mkoani humo. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Kwimba Bw. Seleman Mzee.
Na Mwandishi wetu, Kwimba

Serikali imewahakikishia wakazi wa mji mdogo wa Ngudu Wilayani Kwimba Mkoani Mwanza kuwa hadi kufikia mwezi wa tano mwaka 2014 tatizo la maji katika mji huo litakuwa limekwisha na wakazi wa eneo hilo wategemee kupata maji ya kutosha.

Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe alitoa kauli hiyo hivi karibuni wilayani humo wakati akiweka jiwe la msingi kwa ajili ya mradi wa upanuzi wa mtandao wa maji ya ziwa Victoria kutoka katika kijiji cha Mhalo hadi mji wa Ngudu wilayani kwimba.

“Serikali imefanya kila juhudi kupunguza matatizo ya maji katika wilaya yote ya kwimba na hili leo linaonekana, mradi huu tayari umeshafikia asilimia 60 na ifikapo mwezi wa tano mwaka huu mtaanza kupata maji,” alisema Waziri Maghembe.

Aliongeza kuwa mradi huo wa maji unatokana na ahadi yake aliyompa Rais Jakaya Mrisho Kikwete kuwa katika kipindi cha miezi sita atahakikisha kuwa maji yanafika katika mji wa Ngudu.

“Nilimweleza Rais kuwa katika kipindi cha miezi sita wananchi wa Ngudu watapata maji na kuondokana na adha kubwa wanayoipata na leo ninyi ni mashahidi wa kweli mnaposhuhudia naweka jiwe la msingi kuashiria kumalizika kwa tatizo hili,” aliongeza.

Alisema kiasi cha maji kinachopatikana katika mji wa Ngudu kwa siku ni lita 270, 000 ambazo hazitoshi kukidhi mahitaji ya wananchi kwamba zaidi ya lita 1,000,200 zinahitajika ili kukidhi matatizo ya maji katika eneo hilo.

Alisititiza kuwa kazi iliyobaki mpaka kukamilika kwa mradi huo inaweza kutekelezwa kwa wiki tatu kuanzia sasa na hii ni kutokana na ufanyaji kazi bora unaondelea katika eneo la mradi.

“Umbali wa kutoka katika kijiji cha Mhalo ambako bomba la maji limeanzia mpaka katika mji wa Ngudu ni kilometa 46, kazi kubwa imeshafanyika na ni takribani kilometa 5 ndio zimebaki ili kukamilisha kazi yenyewe, hivyo suala la maji kuingia Ngudu si la kubahatisha,” alisisitiza Profesa Maghembe.

Alisema hadi kukamilika kwake mradi huo utagharimu kiasi cha Tshs bilioni 2.8 na kuwa fedha hizo zimetolewa na serikali ya Tanzania.

“Mradi huu wa upanuzi wa maji kutoka Ziwa Victoria hadi katika mji wa Ngudu ni juhudi za serikali yetu katika kuhakikisha wananchi wake wanapata huduma muhimu kwa wakati,” alifafanua Waziri  wa maji.

Waziri Maghembe aliwaomba wananchi wa Ngudu kuuona mradi huo kuwa ni wa kwao na si wa mtu mwingine, na kuwasihi wautunze ili kuepuka uharibifu unaotokea katika maeneo mengine hapa nchini.

Alisisitiza kuwa watu waache kuvamia vyanzo vya maji na kuwa ni jukumu la wananchi wenyewe kutoa taarifa kwa vyombo husika pale wanapoona uharibifu unafanyika nchi nzima.

“Ni jukumu la kila mtanzania kutunza vyanzo vya maji, kuacha kukata misitu na kwa kufanya hivyo tutalinda vyanzo vya maji, afya zetu na uchumi wetu” alisisitiza.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kwimba, Bw. Seleman Mzee, alitoa shukrani zake za dhati kwa serikali kwa juhudi kubwa ya kupeleka maji katika mji wa Ngudu ambao ulikuwa na tatizo hilo kwa miaka mingi.

“Mji wa Ngudu umekuwa na kilio hiki kwa muda mrefu sana, lakini kutokana na serikali kuwa sikivu, imeliona hilo na leo mmejionea wenyewe Waziri akiweka jiwe la msingi kuashiria ujio wa maji hapa,” alisema Bw. Mzee.

Eneo hilo lenye wakazi 295, 000 limekuwa likitumia maji ya visima ambayo yalikuwa hayakidhi mahitaji ya wakazi wake.

“Mradi huu utakuwa ni mkombozi kwa wakazi wa Ngudu, tunaomba Mh. Waziri upeleke salamu zetu kwa Mh. Rais kuwa kilio tulichokuwa tunakililia kwa muda mrefu sasa kitakwisha,” alisema.


Mwisho  

No comments: