Thursday, April 3, 2014

Bank of Africa Tanzania yatengeneza faida ya Tshs 5.4 bilioni

Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam

Bank of Africa Tanzania imepata faida ya Tshs 5.4 bilioni mwaka 2013 kabla ya kodi ikilinganishwa na faida ya Tshs 3.3 bilioni iliyopatikana mwaka uliotangulia wa 2012.

Faida hiyo ni ongezeko la asilimia 63.

Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Bw. Ammish Owusu-Amoah amesema mafanikio hayo kwamwaka 2013  yanatokana na ongezeko la jumla la kipato cha riba, gharama mbalimbali zinazotozwa pamoja na bidhaa za hazina.

“Ufanisi wa benki kwa mwaka 2013 umeendelea kuwa mzuri na tumeendelea kuwa miongoni mwa benki zinazopata faida Tanzania,” alisema na kuongeza kuwa benki hiyo imeendelea kusaidia wajasiriamali, jamii, kampuni na wateja wake katika matawi yake 19.   

Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo, benki pia imeendelea kubuni huduma mbalimbali hususani kwa ajili ya wateja binafsi.

“Tutaendelea kufanya vyema hasa kutokana na uchumi imara wa Tanzania unaokua kwa asilimia 7,” alisema.

Alifafanua kuwa msisitizo wa benki hiyo kwa mwaka 2014 ni kuongeza mara dufu ufanisi wa benki, kujengea uwezo wafanyakazi na kuongeza ubora wa huduma kwa wateja.

Alisema kutokana na mtazamo huo na bidhaa mpya, benki hiyo ina uhakika wa kuwa moja ya taasisi zitakazotoa majibu ya changamoto zinazowakabili wateja wao pamoja na kuongeza ufanisi. 

“Huduma mbalimbali tulizoanzisha kwa sekta ya umma na binafsi zinalenga kutoa majibu na kukidhi kiu ya wateja wetu, tutaendelea kufanya hivyo,” alisema.

Alisema kuendelea kwa serikali kusimamia sera za kifedha na uchumi mkubwa kama moja ya kutekeleza Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano ilikuwa moja ya sababu za kufikia mafanikio hayo.

Alitaja sababu nyingine kama kushuka kwa mfumuko wa bei hadi kufikia asilimia 5.6 mwezi Desemba mwaka jana.

Pia alisema kuendelea na utafutaji wa gesi na mafuta Tanzania ni fursa nzuri kwa biashara ya benki ambapo huweza kutoa mikopo pamoja na kuongeza wateja wanaoweka akiba zao katikavyombo hivyo vya fedha.


Mwisho

No comments: