Mkuu wa
Idara ya Udhibiti na Tahadhari wa Benki ya Afrika Tanzania, Bi. Mwanahiba Mzee
akimpatia chakula, Bw. Nelson Mwijage kwa ajili ya mgonjwa wake Gilbert
Mtalemwa (aliyelala) katika hospitali ya ya CCBRT mjini Dar es Salaam Jumatatu
wiki hii. Benki hiyo iliandaa chakula cha mchana na kula pamoja na wagonjwa
katika hospitali hiyo kama njia ya kusherehekea nao sikukuu ya Pasaka.
Mkuu wa
Idara ya Udhibiti na Tahadhari wa Benki ya Afrika Tanzania, Bi. Mwanahiba Mzee
akiwaburudisha wagojwa katika hospitali ya CCBRT mjini Dar es Salaam Jumatatu
wiki hii wakati Benki hiyo ilipoandaa chakula cha mchana na kula pamoja na
wagonjwa na wafanyakazi katika hospitali hiyo kama njia ya kusherehekea nao
sikukuu ya Pasaka.
Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Taasisi na watu wenye uwezo wameshauriwa kuongeza
juhudi na kujenga utamaduni wa kusaidia na kuwafariji watu wenye matatizo
mbalimbali wakiwemo wagonjwa mahospitalini ili nao waweze kujisikia na kutambua
kuwa jamii inawajali.
Hayo yalisemwa jijini Dar es Salaam na Mkuu wa Idara
ya Udhibiti na Tahadhari (Head of Risk and Compliance) wa Benki ya Afrika
Tanzania, Bi.Mwanahiba Mzee wakati wafanyakazi wa benki yake walipotayarisha chakula
cha mchana kwa ajili ya kusherehekea sikukuu ya Pasaka na wagonjwa wa hospitali
ya CCBRT Jumatatu wiki hii.
“Ningependa kuona taasisi na watu mbalimbali wanajenga
utamaduni wa kusaidia wenye matatizo ili nao waweze kujisikia kuwa jamii
inawajali,”alisema.
Alisema benki yao kila mwaka inaandaa chakula na kula
na wagonjwa, waganga,wauguzi na wafanyakazi wa hospitali hiyo kama njia ya
kutimiza azma hiyo.
“Hii ni njia ya kuwaletea faraja wagonjwa na hatimaye
kuwasaidia kupata nafuu na kupona haraka,” alisema.
Benki hiyo pia ilitumia fursa hiyo kuwapatia zawadi ya
vifaa vya shule watoto wanaopatiwa matibabu katika hospitali hiyo.
Alieleza kuwa benki yao imejenga utamaduni kila mwaka
wa kutenga sehemu ya faida yake kwa ajili ya kushiriki katika shughuli za
kijamii na hospitali hiyo ni moja ya
taasisi ambazo zipo katika utaratibu wao.
“Mbali ya kuandaa chakula na kula na wagonjwa pia
benki inashiriki katika kuisaidia hospitali hiyo maswala mbalimbali ikiwemo
vifaa,” alisema.
Katika tukio hilo wagonjwa waliburudishwa kwa michezo
mbalimbali ikiwemo ya sarakasi ambayo iliwaburudisha hasa watoto ambao wanakosa
michezo kutokana na matatizo waliyonayo.
Makamu Mkurugenzi wa hospitali, Bi. Brenda Msangi
alisema benki hiyo ni moja ya taasisi ambazo zinashiriki kusaidia hospitali yao
katika maswala mbalimbali.
“Benki hii ni mfano wa kuingwa...tunawashukuru sana,”alisema,
Bi. Msangi.
Alitoa wito kwa taasisi mbalimbali zijenge utamaduni
wa kushiriki katika kuisaidia hospitali hiyo ili iweze kutimiza majukumu yake kwa
ufanisi.
Alisema kuwa hospitali hiyo ina changamoto mbalimbali
na kuwa wanaohitaji matibabu ni wengi hivyo ikisaidiwa itaweza kutimiza
majukumu yake zaidi ya hapo ilipofikia.
Naye Bi. Nyanzobe Goniho ambaye anamuuguza mtoto wake aliishukuru
benki hiyo na kuomba wengine kufuata nyayo za taasisi hiyo ya fedha.
“Tunashukuru sana benki hii kwa kutujali,” alisema Bi.
Goniho.
Mwisho
No comments:
Post a Comment