Na Mwandishi wetu, Pwani
Serikali imesema
imedhamiria kukabiliana kwa vitendo na changamoto ya kutotumia fursa na nafasi
ya kijiografia ya nchi ya Tanzania na kuifanya kuwa shindani na hivyo kuleta
maendeleo endelevu na ustawi wa jamii.
Waziri wa Uchukuzi, Dk.
Harrison Mwakyembe amesema jana mkoani Pwani kuwa hakuna sababu inayoifanya
Tanzania isiwe taifa shindani kibiashara katika ukanda huu wa Afrika kutokana
na nafasi yake kijiografia miongoni mwa sababu nyingine.
Katika kuonyesha dhamira
hiyo kivitendo, Waziri huyo anaongoza ujumbe wa maafisa mbalimbali wa serikali
katika kukagua njia kuu toka jijini Dar es Salaam-Tunduma hadi katika mji wa
Lubumbashi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Barabara hiyo kuu ndiyo
inayotumiwa na magari ya mizigo ya wafanyabiashara wa DRC toka bandari ya Dar
es Salaam, hivyo kwa kukagua maeneo ya mizani, serikali inataka kuondoa kero
zinazowakumba wafanyabiashara hao.
“Tanzania imebarikiwa
kuzungukwa na nchi sita zisizo na bahari na tuna ukanda wa bahari wenye urefu
zaidi ya kilometa 1500…lazima tutumie bahati hii kujiletea maendeleo,”
aliwaambia waandishi wa habari mara baada ya kutembelea kituo cha kupimia
magari cha Maili Moja, Kibaha, mkoani Pwani.
Ziara ya ujumbe huo
ilianzia katika bandari ya Dar es Salaam ambapo Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa
Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Mhandisi Madeni Kipande ulitoa taarifa fupi
kwa Waziri huyo kuhusiana na shughuli bandarini hapo.
Pia ujumbe ulitembelea
Kitengo cha kupakia na kupakua kontena (TICS) bandarini hapo. Maeneo
mengine yaliyotembelewa ni pamoja na bandari za nchi kavu (ICDs) maeneo ya
Kurasini ambapo Waziri alishuhudia msongamano mkubwa wa malori ya mizigo katika
njia hiyo.
“Tunataka kubadilika,
lazima tubadilike,” alisema Waziri Mwakyembe.
Ujumbe huo unaosafiri kwa
barabara ili kupata taarifa za moja kwa moja toka kwa wahusika, unajumuisha pia
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Bw. Peter Serukamba
pamoja na mjumbe wa kamati hiyo, Bi. Zarina Madabida.
Akiongea baada ya kukagua
kituo cha mizani cha Mikese, Bw. Serukamba alisema wanataka kuangalia na
kufahamu kila tatizo kwa kina ili hatimae ufumbuzi wa kudumu upatikane.
“Tuko katika ushindani
mkubwa, lazima kama nchi tubadilike kwa haraka,” alisema Mwenyekiti huyo wa
kamati.
Kwa upande wake, akitoa
mfano wa kasoro zilizopo katika vituo vya kupima mizigo alisema bado muda
unaotumika kushughulikia gari moja ni mrefu na hivyo kupunguza ufanisi.
Waziri Mwakyembe alisema
kasoro hizo pamoja na nyingine zitapatiwa ufumbuzi hivi karibuni kutokana na
mikakati iliyopo.
Ziara hiyo ya kikazi ya
zaidi ya kilometa 2,000 itahitimishwa kwa kufunguliwa kwa ofisi ya TPA Alhamis
wiki hii katika mji wa Lubumbashi ambayo ni moja ya mikakati ya kuongeza
ufanisi wa bandari katika kuhudumia nchi jirani.
Pamoja na maafisa wengine,
ujumbe huo unajumuisha pia maafisa waandamizi toka TPA na Mamlaka ya Usafiri
wan chi kavu na Majini (SUMATRA).
Takwimu za hivi karibuni zinaonyesha kuwa shehena yote ya
mizigo ya nchi 6 zitumiazo bandari ya Dar es salaam, (yaani Zambia, D R Congo,
Burundi, Rwanda, Malawi na Uganda) imeongezeka kutoka tani millioni 3.55 mwaka
2011/12 hadi kufikia tani millioni 4.05 mwaka 2102/13, hiyo ikiwa ni ongezeko
la asilimia 14.2.
Mwisho
No comments:
Post a Comment