Ofisa msajili, Bi. Agnes Maeda(kushoto)
akimsaidia kujaza fomu mmoja wa wa wamiliki wa mabasi ya Daladala Bw. Silas
MlakiSiku katika zoezi la uandikishaji wa mabasi ya abiria kwa Wakala wa Mradi
wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART), ambao mabasi yao yanapita katika
barabara ya Morogoro au kukatiza katika njia hiyo. Zoezi hilo la uandikishaji
lilianza jumatatu kwenye ofisi za wakala Ubungo Plaza jijini Dar es Salaam.
Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Siku tatu tangu kuanza kwa zoezi la uandikishaji wa
mabasi ya abiria kwa Wakala wa Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART), wamiliki
wa vyombo hivyo vya usafiri wamendelea kujitokeza kwa wingi kama moja ya
michakato ya kufanikisha awamu ya kwanza ya mradi huo.
Wamiliki
wote wa mabasi hayo ya abiria maarufu kama daladala ambao mabasi yao yanapita
katika barabara ya Morogoro au kukatiza katika njia hiyo walianza zoezi hilo katika
ofisi za wakala huo Jumatatu wiki hii.
Mshauri Mwelekezi wa wakala huo, Bw. Felix Mlaki
aliwaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana kuwa zoezi hilo linalotarajia
kuchukua siku 22 linaendelea vyema na kwamba wamiliki wa daladala wameendelea
kujitokeza kwa wingi kujiandikisha.
“Zoezi zinaendelea vizuri na sisi tunawapongeza kwa
mwitikio wao na tunazidi kuwaomba wale ambao bado hawajafika waendelee kuja
kujiandikisha,”alisema Bw. Mlaki.
Alisema kuja kwao pia kunasaidia wakala wa mradi
kupata maoni yao ambayo yatasaidia katika kuuwezesha mradi huo kufikia malengo
yake.
Aliongeza kusema kuwa zoezi la kujiandikisha
linafanyika bila malipo yoyote hivyo watu waendelee kushiriki katika zoezi
hilo.
Alifafanua kuwa mradi huo ni mkubwa sana na ni wa kisasa
hivyo wamiliki wa daladala hawana budi kutoa ushirikiano wao ili mwishoni mwa
mwaka huu uweze kuanza kufanya kazi.
Aliwasistiza wenye daladala kuzidi kutumia muda
uliopangwa vizuri katika kujiandikisha ili zoezi liweze kukamlika kwa muda
uliopangwa.
Kwa sasa wakala huo uko kwenye mchakato wa kuwezesha
upatikanaji wa watoa huduma kwenye mfumo mpya wa mabasi yaendayo haraka awamu
ya kwanza ambayo inajumuisha barabara ya Morogoro, Kawawa na mtaa wa Msimbazi
kwa njia kuu na nyingine za kiungo.
Kulingana na mpango wa uendeshaji wa mfumo wa DART,
barabara zinazohusika zitapaswa kutumiwa na mabasi ya mfumo huo pekee.
Jumla ya njia 64 zitakoma kutumika baada ya mradi huo
kuanza.
Awali, wakala huo ulitangaza muda wa kujiandikisha kwa
siku za Jumatatu hadi Ijumaa kuwa ni kuanzia saa tatu asubuhi mapaka saa 11
jioni na siku za Jumamosi na Jumapili ni kuanzia saa tatu asubuhi hadi saa nane
na nusu mchana.
“Tunahitaji zoezi hili likamilike katika kipindi kilichopangwa
ili mradi uanze kwa wakati,”alisema Bw. Mlaki.
Awamu ya kwanza ya mradi huo inahusisha barabara ya
Morogoro, Kawawa na mtaa wa Msimbazi kwa njia kuu na njia za nyingine za
kiungo.
Wakala wa DART ni chombo kilicho chini ya Ofisi ya
Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).
Mwisho
No comments:
Post a Comment