Na Mwandishi wetu, Mwanza
Katika kuhakikisha inatekeleza sera ya maji hapa nchini
serikali imedhamiria kufanya mabadiliko makubwa ya kupeleka maji katika maeneo
mengi vijijini katika kipindi cha kuanzia Juni mwaka huu hadi mwishoni mwa mwaka
2015.
Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Mghembe aliyasema hayo
hivi karibuni jijini Mwanza wakati akizungumzia sera ya maji na utekelezaji
wake katika kuwafikia wananchi katika maeneo ya vijijini na mijini.
“Kupitia wizara ya maji serikali
imeanzisha miradi mbalimbali ya maji hapa nchini, hii yote ni katika kutekeleza
sera ya maji ambayo inasema kila mwananchi angalau asiishi umbali wa mita 400
kutoka eneo la maji yanakopatikana,” alisema Waziri wa maji.
Aliongeza kuwa upatikanaji wa maji nchini umegawanyika
katika mafungu matatu, fungu la kwanza
ni upatikanaji wa maji kwenye miji mikuu ya mikoa na jiji la Dar es Salaam,
upatikanaji wa maji vijijini na tatu ni upatikanaji wa maji katika miji midogo
na miji mikuu ya wilaya.
“Katika miji mikuu ya mikoa na Dar es Salaam wastani wa
upatikanaji wa maji ni asilimia 88 kama ilivyoelezwa kwenye sera ya maji,
lakini ziko tofauti kutoka mji mmoja hadi mwingine,” alisema.
Alisema kwa maeneo ya vijijini upatikanaji wa maji bado uko
chini, takwimu zikionyesha kuwa ni kama asilimia 49.
“Tunategemea kwamba mpaka kufikia mwezi Juni mwaka huu
tutafika asilimia 55 na kufikia asilimia 74 ifikapo mwezi Desemba mwaka 2015,”
alisema.
Alifafanua kuwa katika maeneo ya miji mikuu ya wilaya na
miji midogo kama Mombo, na miji mikuu kama Muheza, Korogwe, Mwanga, Magu, Lamadi,
Chato, Makambako, na Tunduru upatikanaji
wa maji ni ni wastani wa asilimia 51.5.
Alisema kutokana na hali hiyo mwaka huu wizara imechukua
hatua ya kwanza ya kuhakikisha kwamba serikali inabadilisha hali hiyo, huku
akisema lengo la sera ya maji ni kwamba kufikia mwaka 2015 katika miji midogo
maji yawe yamefika kwa asilimia 55.
Aliongeza kua hivi sasa wizara yake inatekeleza miradi
1600 ambapo pamoja na matatizo ambayo wanakumbana nayo ya kifedha bado miradi
mingi imekamilika.
Alisema kutokana na changamoto za maji nchini, serikali
kupitia wizara yake inajitahidi kutekeleza miradi mbalimbali kwa haraka kama
moja ya mikakati ya kufikia maendeleo miongoni mwa jamii.
Mapema katika ziara yake mkoani humo, Waziri Maghembe alitoa
rai kwa watanzania kulinda vyanzo vya maji na kuwasihi kutunza miundombinu ya
maji.
“Ni jukumu la kila mtanzania kutunza vyanzo vya maji,
kuacha kukata misitu na kwa kufanya hivyo tutalinda vyanzo vya maji, afya zetu
na uchumi wetu” alisisitiza.
Mwisho
No comments:
Post a Comment