Na Mwandishi wetu,
Dar es Salaam
Katika juhudi za
kuimarisha hali ya usafiri na kupunguza msongamano, alama mpya za barabarani na
mabadiliko ya njia yanategemewa katikati ya jiji la Dar es Salaam kuanzia
mwishoni mwa mwezi huu.
Kuanzia tarehe 28
mwezi huu, uongozi wa jiji hilo utaanza kuondoa alama za zamani na kuweka mpya
katika maeneo mbalimbali ya katikati ya jiji hilo.
Akielezea
mabadiliko hayo jijini Dar es Salaam jana, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ilala,
Bw. Jerry Silaa alisema mabadiliko hayo yanaendana na matakwa ya utaratibu mpya
wa usafiri wa mabasi yaendayo haraka yanayotarajiwa kuanza mwishoni mwa mwaka
huu.
“Patakuwa na
mabadiliko ya njia na alama mpya ambavyo vitapaswa kufuatwa na kuheshimiwa na madereva
wote wa magari na vifaa vingine vya moto,” aliwaambia waandishi wa habari jana.
Bw. Silaa alisema
mbali na kuhakikisha utaratibu wa mabasi yaendayo haraka unatekelezeka ipasavyo
na kwa ufanisi, mabadiliko hayo pia yanalenga kimsingi kupunguza msongamano
katikati ya jiji.
Pia mabadiliko
yanalenga kuongeza ufanisi wa ufanyaji kazi wa mabasi ya daladala na kutoa
nafasi kwa baadhi ya eneo la barabara ya Morogoro kubakia kuwa kwa ajili ya
mabasi yaendayo haraka na waenda kwa miguu tu.
“Watu wanatakiwa kufahamu mabadiliko haya hasa wanapoendesha
magari kuja katikati ya jiji,” alisema.
Akielezea zaidi mabadiliko hayo, mwakilishi wa Halmashauri ya Ilala
Kwenye Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT), Mhandisi Tigahwa Serapion alisema
mabasi yote yanayopita barabara ya Kilwa yataishia Stesheni na kurudi kupitia
njia hiyo hiyohiyo, huku yale yanayopita barabara ya Nyerere na Uhuru yataishia
kituo cha Mnazi Mmoja na kurudi kupia njia zao.
Pia kutakuwa na mabasi yatakayoanzia Mnazi Mmoja kupitia njia ya Bibi Titi,
Maktaba hadi kituo cha Posta ya zamani Benki ya NBC na kurudi kupitia njia
hiyohiyo.
Bw. Serapion alisema mabasi yote yanayopita barabara ya Ali Hassan
Mwinyi kuelekea katikati ya jiji yataishia katika kituo cha YMCA barabara ya
Upanga na kurudi kupitia njia hiyohiyo.
Alisema pia barabara ya Sokoine zitaruhusiwa gari binafsi kupita
kuanzia Kituo cha Kati cha Polisi (Central Police) kuelekea Kivukoni, Hospitali
ya Ocean Road hadi kwenda kuungana na barabara nyingine ikiwemo ya Ali Hassani Mwinyi.
Kwa upande wa barabara ya Samora, badala ya kwenda hadi Hosptali ya
Ocen Road sasa gari ndogo binafsi zitaanzia katika hospitali hiyo kwenda Mnara
wa Saa (Clock Tower).
Alisema njia zote za mabasi hayo ya daladala hazitakatiza katika
barabara ya maradi wa BRT isipokuwa yale yanayotoka Mnazi Mmoja kwenda Posta ya
Zamani.
Alisema alama zitawekwa kuonyesha njia hizo zitakavyokuwa na namna
mabasi yanayotoka Mnazi Mmoja yatakavyoweza kukatiza katika barabara ya mradi
huo wa mabasi.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment