Tuesday, April 22, 2014

Waziri Mbene ahamasisha uwekezaji katika maeneo maalumu ya EPZA

Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam

Serikali imewahamasisha wawekezaji wa ndani na nje kuwekeza kwa wingi katika maeneo ya Mamlaka ya Ukanda Maalumu wa Uwekezaji nchini (EPZA) kwa faida yao na ya nchi kwa ujumla.

Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Bi. Janeth Mbene amesema uwekezaji katika maeneo hayo una uwezo mkubwa wa kuongeza uzalishaji wa bidhaa kwa masoko ya nje na hivyo kukuza uchumi wa nchi kwa haraka.

Waziri huyo alikuwa akitembelea Kiwanda cha Tanzania Tooku Garments Co. LTD ambacho kiko katika eneo la EPZA jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.

“Maeneo haya yana fursa nyingi ambazo wawekezaji wanaweza kufaidika nazo...nawahamasisha waje kwa wingi na serikali itawasaidia kuweka mazingira bora zaidi,” alisema Bi. Mbene.

Kiwanda hicho kinatengeneza nguo kwa ajili ya soko la nje ya nchi.

“Nina furahi kuona kiwanda hiki kimetoa ajira kwa watanzania wengi...haya ndiyo mambo ambayo serikali inapigania wakati wote,” aliongeza kusema.

Kabla ya kufanya ziara katika kiwanda hicho, Naibu Waziri huyo alikutana na watendaji wa EPZA na kufanya nao mazungumzo.

Katika mazungumzo yao, aliwahakikishia watendaji na viongozi wa mamlaka hiyo kuwa serikali itaendelea kushirikiana nayo vyema katika kusukuma gurudumu la maendeleo.

Naye Meneja Mkuu Msaidizi wa Tanzania Tooku Garments CO.LTD, Bw. Rigobert Massawe alisema kiwanda hicho kinazalisha nguo aina ya jeans na tisheti kwa ajili ya masoko ya nje.

“Hiki ni kiwanda kikubwa cha nguo na masoko yake yapo katika nchi mbili za Marekeni na Uingereza,”alisema Bw. Massawe.

Alisema kwa sasa wanatumia zaidi soko la Marekani na baada ya maboresho zaidi watauza katika soko la Uingereza.

Kwa mujibu wa Meneja huyo, kiwanda kimeajiri watanzania zaidi ya 800 na kuwa katika malengo ya kiwanda kufikia mwaka 2025 kitaweza kuajiri watu 15,000.

Akiongea hivi karibuni, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo, Dkt. Adelhelm Meru alisema mamlaka yake imedhamiria kuona uwekezaji unakua na kuchangia maendeleo ya nchi hasa kupitia viwanda.

Alisema Tanzania inahitaji wawekezaji ili kufikia malengo ya maendeleo iliyojiwekea na kuwa mamlaka yake itaendeleza juhudi za kuvutia wawekezaji hao.

“Tutaendeleza juhudi hizi kwa faida ya nchi yetu, nchi nyingi ambazo zimeendelea zimetumia njia hii kufikia maendeleo,” alisemaDkt Meru alisema uongozi wa EPZA umefanya juhudi kubwa kuhamasisha wawekezaji wa ndani kutumia fursa zilizopo katika mifumo ya EPZ na SEZ ambapo kwa sasa tayari makampuni ya ndani yameanza kujitokeza kwa wingi.

Alieleza kuwa kati ya makampuni 113 yaliyojenga viwanda kupitia EPZA, asilimia 44 ni makampuni ya ndani, ambapo asilimia 14 ni ya ubia kati ya makampuni ya ndani na ya nje na asilimia 42 ni makampuni ya nje.

Ni katika wiki chache zilizopita ambapo EPZA ilitoa leseni mpya kwa kampuni mpya 13 ambazo zinatarajia kwa pamoja kuwekeza mtaji wa dola za Kimarekani milioni 62.2 na kutoa ajira takribani 3,500 kwa watanzania. 

Pia kampuni hizo zinatarajia kuuza nje bidhaa zenye thamani ya dola milioni 61.86 kwa mwaka.

Dkt. Meru alisema kuwa katika juhudi za kuhamasisha uwekezaji katika kipindi cha miezi mitatu ya Januari hadi Machi mwaka huu wameweza kusajili makampuni hayo yakiwa yanatokea katika nchi mbalimbali na Tanzania ikiwa mojawapo.

Mwisho


No comments: