Thursday, June 5, 2014

Maafisa, wafanyabiashara wa jimbo la Katanga watua Dar kuimarisha uhusiano

Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam

Katika hatua ya kuimarisha zaidi uhusiano wa kibiashara kati ya Tanzania na nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ujumbe wa serikali ya Jimbo la Katanga na wafanyabiashara wamewasili nchini.

Ujumbe huo wa watu 16 unaongozwa na Naibu Gavana wa jimbo hilo, Bw. Yav Guilbert na Waziri wa Uchukuzi wa Jimbo hilo, Bw. Kahozi Sumba.

Akiongea na waandishi wa habari mara baada ya kuwapokea katika uwanja wa ndege jijini Dar es Salaam Jumatatu usiku, Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe alisema ziara hiyo inalenga kuimarisha uhusiano kati ya pande hizo mbili.

“Tunataka kumaliza mazungumzo tuliyoaanza ili kuimarisha mahusiano yetu,” alisema.

Mwanzoni mwa mwezi wa Tano mwaka huu, Tanzania ilifungua ofisi ndogo ya mawasiliano ya Mamlaka ya Bandari (TPA) mjini Lubumbashi katika jimbo hilo la Katanga.

Ofisi hiyo inalenga kurahisisha na kuleta ufanisi katika kusafirisha mizigo ya wafanyabiashara wa Kongo wanaotumia bandari ya Dar es Salaam.

Ofisi hiyo mpya inalenga kusaidia wafanyabiashara wa DRC kumaliza matatizo yao Lubumbashi badala ya kusafiri hadi Dar es Salaam.

Mienendo ya taarifa za mizigo itafanyika mjini humo na hivyo kuharakisha taratibu za mizigo bandarini Dar es Salaam.

Waziri Mwakyembe alisafiri kwa barabara tokea Dar es Salaam hadi Lubumbashi kupitia Zambia kwa barabara zaidi ya kilometa 2000 kuangalia na kupata taarifa za changamoto wanazokumbana nazo wafanyabiashara wa DRC kuanzia bandarini Dar es Salaam hadi njiani wanaposafiri.

Kwa upande wake, Gavana Guilbert, aliishukuru serikali ya Tanzania kwa mapokezi mazuri waliyopata.

“Tunashukuru sana kwa mapokezi…tunajisikia nyumbani,” alisema.

Katika ziara yao, ujumbe huo ulitarajiwa jana kutembelea maeneo mbalimbali yakiwemo bandari pamoja na kuongea na maafisa wa serikali ya Tanzania.

Mizigo ya DRC imekuwa ikiongezeka kwa asilimia takribani 24 kwa mwaka tangu mwaka 2004 ikiongezeka toka tani 155,611 hadi tani 1,117,249 mwaka 2013.

Nchi ya DRC ni ya pili kwa kupitisha mizigo mingi katika bandari ya Dar es Salaam.  kwa mujibu wa takwimu zilizopo, mizigo ya DRC inachukua asilimia 25 ya mizigo yote ya nchi jirani inayopita katika bandari hiyo.

Mwisho



No comments: