Wednesday, June 18, 2014

Benki ya Afrika Tanzania yafadhili wawili mkutano wa kimataifa wa biashara

 Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Afrika Tanzania, Bw. Ammish Owusu – Amoah (kulia) akimpa mkono kama ishara ya kumpongeza mmoja wa wafanyabiashara, Bw. Emmanuel Mallya wa pili kutoka kushoto wanaokwenda nchini Moroko kudhuria mkutano mkubwa wa wafanyabiashara kutoka katika mataifa 17 Barani Afrika, ambapo benki hiyo ina matawi yake, wafanyabiashara hao wawili wamefadhiliwa na Benki hiyo kwenda kushiriki katika mkutano huo unafanyika kati ya tarehe 24 – 25 juni 2014, nchini Moroko. Wengine katika picha ni Godwin Makyao mfanyabiashara wa pili kutoka kulia na Chanja Mwombela wa kwanza kutoka kushoto ambaye ni mkuu wa idara inayoshuhulikia wafanyabiashara.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Afrika Tanzania Bw. Ammish Owusu – Amoah ( kulia) akibadilishana mawazo na wafanyabiashara, Godwin  Makyao katikati na Emmanuel Mallya wa kwanza kushoto, wafanyabiashara hao wanakwenda nchini Moroko kudhuria mkutano mkubwa wa wafanyabiashara kutoka katika nchi 17 barani Afrika ambazo benki hiyo inamatawi yake, wafanyabiashara hao wawili wamefadhiliwa na Benki hiyo kwenda kushiriki katika mkutano huo unafanyika kuanzia tarehe 24 – 25 juni 2014 nchini Moroko.
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Kujenga mitandao ya kibiashara na kujifunza kutoka kwa wengine imetajwa kama moja ya njia muhimu zitakazowasaidia wafanyabiashara wa Tanzania kufanikiwa katika sekta za biashara na uwekezaji.

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Afrika Tanzania, Bw. Ammish Owusu – Amoah alitoa ushauri huo jijini Dar es Salaam jana, wakati wa kuwaaga wafanyabiashara wawili waliofadhiliwa na benki hiyo kwenda nchini Morocco kudhuria mkutano mkubwa wa wafanyabiashara kutoka katika mataifa 17 barani Afrika.

“Benki yetu inaona wateja wetu kama familia moja na lengo letu ni kukua pamoja, hivyo msaada huu utasaidia wao kuongeza uzoefu katika biashara hasa wanapokutana na wafanyabiashara wa nchi nyingine,” alisema Mkurugenzi huyo.

Alisema kuwa mkutano huo utakaofanyika kuanzia tarehe 24 – 25 utatoa mwanga mkubwa kwa wafanyabiashara hao wakitanzania kupata fursa mbalimbali katika sekta ya biashara na uwekezaji kutoka katika nchi ambazo benki hiyo ina matawi yake.

“Hii ni fursa ya pekee kwa wenzetu hawa kuitangaza nchi katika mkutano huo mkubwa, kwani itasaidia kuwavuta wawekezaji wapya kupitia wafanyabiashara hawa,” alisisitiza.

Aliongeza kuwa anamini mafanikio ya wafanyabiashara hao si tu yatafaidisha kampuni zao bali hata benki na nchi kwa ujumla katika kukuza uchumi.

Mkutano huo pia utahudhuriwa na wafanyabiashara kutoka katika nchi ya China.

“Nchi ya China inajulikana kwa kufanya biashara na uwekezaji katika nchi mbalimbali duniani, hii itakua fursa nyingine kwa wafanyabiashara hawa kukutana nao na kuwaelezea fursa za uwekezaji zilizopo hapa Tanzania,”aliongeza.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa EB Maritime Group inayojishughulisha na usafirishaji wa mizigo, Bw. Emmanuel Mallya alisema fursa hiyo ni kubwa sana kwao na wanaiona kama ni njia muhimu ya kuweza kuitangaza nchi katika sekta za biashara na uwekezaji.

“Kwa sisi ambao tunajishughulisha na usafirishaji, ni muhimu sana kuhudhuria mikutano mikubwa ya kibiashara kwa sababu tunakutana na wafanyabiashara wa aina mbalimbali,” alisema Mallya.

Alisema wataituimia fursa hiyo vyema kama inavyotakiwa.

Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Maktech Telecommunications, Bw.Godwin Makyao alisema hawaendi kuangalia soko kutoka nchini China pekee bali hata kwa nchi zilizoko magharibi mwa Afrika ambazo bado hazijafahamu fursa zilizopo Tanzania.

“Kwa sisi ambao tunajishughulisha na masuala ya mawasiliano ni njia pekee ya kukutana na wenzetu wa Afrika Magharibi na Kaskazini na kupeana uzoefu katika nyanja hii muhimu kwa dunia ya sasa,”alisema.

Aliongeza kuwa siku zote watu wanahitaji teknolojia mpya hasa katika sekta ya mawasiliano, huku akisisitiza kuwa Tanzania ndio kwanza inaendelea kuwekeza nguvu katika sekta ya habari na mawasiliano hivyo nafsi kama hizo ni adimu kwa baadhi ya wafanyabiashara kushiriki na kujifunza.

“Kutembea ni kujifunza mengi…tutawakilisha vizuri na tutarudi na mawazo mapya,”alisistiza Makyao.

Mwisho.


No comments: