Thursday, June 5, 2014

TTCL yazidi kujiimarisha Pemba

Mkuu wa Kitengo cha Ufundi, Mtandao na Ukarabati wa Kampuni ya Mawasiliano Tanzania (TTCL), Bw. Jothan Lujara(kushoto) na Mkuu wa Mkoa Kusini Pemba, Bw. Juma Kasim Tindwa wakifuatilia jambo wakati wa uzinduzi wa ujenzi wa jengo la TTCL visiwani Pemba hivi karibuni.  TTCL inajitanua visiwani humo na nchi nzima katika juhudi za kuimarisha huduma zake.
Na mwandishi wetu, Pemba
Katika harakati za kujiimarisha nchi nzima, Kampuni ya Mawasiliano Tanzania (TTCL) imeanza ujenzi wa ofisi ya kisasa ya huduma kwa wateja katika eneo la Madungu, Chakechake Pemba litakalo ghalimu Tshs. bilioni 1.2.

Akiongea kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, Dr. Kamugisha Kazaura, Mkuu wa Kitengo cha Ufundi, Mtandao na Ukarabati, Bw. Jothan Lujara aliwambia waandishi wa habari visiwani Pemba hivi karibuni kuwa kampuni yao inaanza ujenzi katika eneo hilo kama njia ya kujiimalisha katika utoaji huduma visiwani humo na nchi nzima kwa ujumla.

“Kwa muda mrefu, tulikuwa tukitoa huduma zetu kwa wateja kwa kutumia jengo la kukodi katika eneo hili na sasa tumeamua tuwe na jengo letu,”alisema.

Alisema kati ya fedha hizo, Tshs 1.1 bilioni atalipwa mkandarasi atakaye jenga jengo hilo na na Tshs 93 milioni atalipwa mshauri mwelekezi wa ujenzi.

“Fedha zote hizi zinagharimiwa na kampuni yetu kutokana na vyanzo vyake vya mapato,”alisema.

Jengo hilo litakuwa na ghorofa moja na inalenga kupunguza gharama za uendeshaji.

Alisema mchakato wa zabuni uliipata kampuni ya MS Quality Building Contractors Limited kufanya kazi hiyo wakati kampuni ya MS Inter Consult Ltd ilipatikana kuwa mshauri mwelekezi wa ujenzi huo.

Inatarajiwa kuwa mkandarasi atajenga jengo hilo kwa kipindi cha miezi nane na mategemeo ni kuwa mwisho wa mwezi wa Februari 2015 jengo litakuwa limekamilika.

Mkuu wa Mkoa Kusini Pemba, Bw. Juma Kasim Tindwa alisema jengo hilo litasaidia kutoa huduma nzuri Chakechake Pemba kwa vile linajengwa kisasa na lenye nafasi kubwa.

“Leo naikabidhi kampuni ya MS Quality Building Contractors Ltd ili ianze rasmi ujenzi huu na matarajio yangu itamaliza kwa wakati,”alisema.

Alisem sifa kubwa kwa makandarasi ni kujenga kwa ubora na kukamilisha kwa wakati ili iweze kupata sifa zaidi.

Alisema anaamini kuwa kukamilika kwa ujenzi huo kutaondoa usumbufu uliokuwepo sababu jengo hilo litazidi kutoa ari ya kufanya kazi kwa viwango. 

No comments: