Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Dk.
Reginald Mengi (kushoto) akielezea jambo kwa Mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi
wa Kituo cha Uwekezaji nchini (TIC), Prof. Lucian Msambichaka (katikati) na
Mkurugenzi Mstaafu wa TIC na pia Balozi wa heshima wa Botswana hapa nchini,
Eng. Emmanuel Ole Naiko wakati wa kongamano la pili la biashara kati ya Tanzania
na China lililomalizika hivi karibuni jijini Dar es Salaam.
Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Wafanyabiashara wa Tanzania wameshauriwa kutumia fursa
waliyopata wakati wa kongamano la pili la biashara kati ya Tanzania na China
kujenga mtandao wa kibiashara utakaodumu kwa faida yao na nchi kwa ujumla.
Akiongea na waandishi wa habari katika siku ya mwisho ya
mkutano huo jana, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji nchini (TIC), Bi.
Juliet Kairuki alitoa wito kwa wafanya biashara wa Tanzania kutumia mahusiano waliyojenga
katika kongamano hilo ili kujiimarisha kimataifa.
“Fursa hii ikitumika vyema, itasaidia wafanyabiashara
wetu kukuwa na hivyo kuongeza mapato katika nchi yetu kwa kuvutia mitaji,
teknolojia na ujuzi,” alisema.
Alisema wafanya biashara wa nchi hiyo wapo tayari
kufanya biashara na watanzania ambao alisema wanatakiwa kuchangamkia fursa hiyo
waliyoipata.
Katika kongamano hilo, TIC pamoja na taasisi nyingine
zilipata nafasi kutangaza fursa za biashara na uwekezaji Tanzania na pia
wafanyabiashara wa pande zote walifanya mkutano wao kufahamiana na kuona
uwezekano wa kufanya kazi pamoja.
Tanzania ilijinadi katika maeneo mbalimbali kama
miundombinu, Kilimo, utafutaji mafuta na uchimbaji gesi, viwanda, madini na
biashara.
Bi. Kairuki alisema kuwa nchi inahitaji mitaji mingi
kutoka nje ya nchi (FDI) na wafanya biashara wa nchi hiyo ya pili kwa uchumi
duniani wanahitajika zaidi kuja kibiashara nchini.
“Mitaji ya kutoka nje ya nchi inasaidia kukuza mapato
na uchumi ndiyo maana kituo chetu kinafanya kazi ya kuvutia wawekezaji,”
alisema.
Alisema kampuni zilizoshiriki kongamano hilo ni zenye uwezo
mkubwa wa kimitaji kuwekeza katika sekta mbalimbali na kwamba Tanzania iko
tayari kufanya nao kazi na kuwa itaendelea kuweka mazingira mazuri ya biashara
ili kuzidi kuvutia wawekezaji.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa bodi wa Kituo
hicho,Profesa Lucian Msambichaka alisema wawekezaji wamekuja katika wakati
mwafaka ambao taifa linawahitaji.
“Tunatambua bila uwekezaji hakuna maendeleo ndiyo maana
hata nchi nyingi duniani zinavutia wawekeji na mitaji,” alisema.
Alisema huu ni wakati wa wafanyabiashara wa Tanzania
kushirikiana na wale wa China ili kukuza mapato yao na uchumi wa taifa.
Alisema kituo kituo cha uwekezaji kimejipanga kuzidi
kushirikiana na wafanyabiashara wa ndani na nje ili kukuza uwekezaji.
Mmoja wa wawekezaji kutoka China, Bw. Kendall, alisema
amefurahishwa na taarifa kuhusu Tanzania alizopata katika kongamano.
“Tanzania inaweza kufikia hatua kubwa ya maendeleo
baada ya miaka 10 au 20...mwenendo wa nchi hii unaridhisha,” aliwaambia
waandishi wa habari.
Hata hivyo, alisema ili hilo litokee panahitajika
kuwepo sera ya kuwawezesha wananchi kielimu pamoja na ufundi katika Nyanja
mbalimbali na kwa madaraja tofauti hasa ya chini na kati.
“Elimu na maarifa ya ufundi kwa watu wengi ni muhimu
kama nchi inataka kupata maendeleo ya haraka,” alisema.
Kongamano hilo lilishirikisha kampuni zaidi ya 100
kutoka China na kampuni zaidi ya 120 za kitanzania.
Hadi sasa China imesajili miradi 522 TIC yenye thamani
ya dola za Kimarekani bilioni 2.4 ambayo inatarajiwa kuzalisha ajira 77,335.
Kongamano hilo la siku tatu liliandaliwa na TIC kwa
kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na Baraza la
Biashara China Afrika (CABC) na kudhaminiwa na Stanbic Bank Tanzania.
Kongamano hilo lilifunguliwa na Makamu wa Rais wa
China Bw, Li Yuanchao.
Mwisho
No comments:
Post a Comment