Na
Mwandishi wetu, Dar es Salaam
KAMPUNI
ya ujenzi ya Strabag International GmbH inayojenga barabara ya Mradi wa Mabasi
yaendayo Haraka (DART) imetangaza mabadiliko ya muda katika eneo la Ubungo
kuanzia kesho na keshokutwa usiku kutokana na ujenzi unaoendelea wa barabara.
Akiongea
na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam jana,Ofisa Uhusiano wa kampuni
hiyo, Bwana Yahya Mkumba, alisema kazi hiyo itahusu ujenzi katika makutano
ya barabara za Morogoro, Sam Nujoma na Nelson Mandela katika eneo la Ubungo.
Alisema
ujenzi huo utakaoanza leo utasababisha kufungwa kwa baadhi ya njia katika
barabara hizo kuanzia saa nne usiku hadi saa 12 asubuhi kesho Jumamosi.
Akielezea
zaidi alisema katika awamu ya kwanza ujenzi huo utahusisha eneo la upande wa
kulia la makutano la barabara ya Sam Nujoma na Morogoro ambalo litafungwa.
“Hali hii
itasababisha magari yanayotoka maeneo ya Buguruni na Tabata kuelekea maeneo ya
Mwenge kutoweza kutumia njia ya Sam Nujoma watakapofika taa za Ubungo,”
alisema.
Alifafanua
kuwa magari hayo yatalazimika kufuata alama zitakazowaelekeza kupita katika
barabara za mradi zinazojengwa hadi barabara ya Shekilango ambapo wataweza
kukutana tena na Sam Nujoma kwa kutumia barabara ya Igesa.
Pia
magari yatakayokuwa yanatokea Sinza kupitia barabara ya Igesa hayataweza
kuelekea eneo la Ubungo yatakapofika katika makutano ya barabara za Igesa na
Sam Nujoma.
Alifafanua
kuwa magari yanayotumia barabara ya Morogoro kutokea maeneo ya Mbezi na Kimara
yatalazimika kuchepuka kulia na kutumia barabara za mabasi ya mwendo wa haraka
yatakapofika eneo la Kibo ambapo patakuwa na kizuizi.
Bw.
Mkumba alisema katika awamu ya pili ya ujenzi huo, eneo la upande wa kushoto la
makutano ya barabara za Morogoro na Nelson Mandela litafungwa siku ya Jumamosi
kuanzia saa nne usiku hadi saa 12 asubuhi siku ya Jumapili.
Katika
awamu hii, alisema, watumia magari yatakayokuwa yanatokea eneo la Mwenge
kutumia barabara ya Sam Nujoma yatalazimika kuchepuka kushoto kukamata barabara
ya Igesa kisha Shekilango.
Pia
magari yatakayokuwa yanatokea barabara ya Nelson Mandela na kutaka kuelekea
mjini kwa kutumia njia ya Morogoro yatalazimika kuchepuka kushoto na kwenda
kugeukia eneo la Kibo ili kuikamata barabara ya Morogoro.
“Tunaomba
radhi kwa usumbufu wowote utakaotokea,” alisema Bwana Mkumba na kuongeza kuwa
pamoja tunajenga na hivyo usumbufu utakuwa ni wa muda mfupi.
Mradi wa
Mabasi yaendayo haraka unatarajiwa kuondoa adha ya foleni katika jiji hilo na
kuleta ufanisi wa usafiri.
Mwisho
No comments:
Post a Comment