Tuesday, June 24, 2014

Benki ya Wanawake yazidi kujitanua

Na Mwandishi Wetu, Njombe

Katika juhudi za kuhakikisha kuwa lengo la serikali la kuwafikishia huduma bora za fedha wananchi wengi kadiri inavyowezekana linafikiwa, Benki ya Wanawake Tanzania imezidi kufungua matawi zaidi.

Akiongea wakati wa ufunguzi wa tawi jipya Makambako mkoa wa Njombe hivi karibuni, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo, Bi. Margreth Chacha alisema benki hiyo imedhamiria kusambaza huduma zake nchi nzima.

“Benki imejipanga kutoa huduma hizi  kwa vile ni asilimia 12 tu ya watanzania wanaopata huduma za kibenki na sehemu kubwa kati ya hao ni watu waishio mijini hasa wanaume,”alisema.

Alisema benki hiyo inalenga watu wa kipato cha chini hasa wanawake ili waweze kukuza shughuli zao za kijasiriamali.

Pamoja na hayo, alisema benki inakabiliwa na changamoto  mbalimbali ikiwemo ya mtaji ambapo ina mtaji wa Tshs bilioni 8.3 ambao ni kidogo kuweza kufikia malengo yake kwa wakati.

Pia aliomba Serikali iharakishe upimaji wa aridhi nchini kote hasa vijijini ili kuwawezesha wananchi hasa  wanawake kupata dhamana kwa ajili ya mikopo.

Kwa sasa, benki hiyo inatoa huduma zake katika mikoa ya Mwanza, Dodoma, Ruvuma, Iringa, Mbeya na sasa Makambako mkoani Njombe.

Kwa upande wake, Naibu Waziri, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Dkt. Pindi Chana aliwataka wajasiriamali katika wilaya hiyo kutumia vizuri mikopo watakayopata toka benki hiyo kwa makini ili waweze kukuza mitaji ya biashara yao hatimaye iweze kusaidia harakati za kupambana na hali duni ya maisha na kukuza uchumi wa nchi.

“Kumbukeni mikopo siyo zawadi bali inahitaji kurejeshwa kulingana na masharti, sasa ni vema ikatumika kwa ajili ya kukuza mitaji ya biashara,”alisema,Dkt. Chana.

Alisema benki hiyo inafanya kazi kubwa ya kutoa mafunzo ya ujasiriamali na mikopo kwa njia ya vikundi bila kuhitaji dhamana, hivyo fursa hiyo waitumie vizuri.

Benki hii kwa kiasi kikubwa imekuja kusaidia shughuli za wajasilimali ambapo hadi sasa imeshatoa fedha zenye thamani ya zaidi ya Tshs bilioni 36 kwa wafanya biashara nchini.

“Hatua hii inatia moyo kuwa chombo chetu kinafanya kazi kubwa ya kupambana na adui mkubwa umaskini unaosumbua jamii,”alisema.

Alisema juhudi zinazofanywa na benki hiyo ni za kuigwa kwa vile nchi haiwezi kujivunia maendeleo kama wananchi wake bado hawana vipato vya kuwawezesha kukidhi mahitaji ya kila siku.

Alisema serikali inatilia mkazo sana swala la kukuza ujasiriamali sababu kupitia shughuli za kibiashara, pato la taifa linakua na baadaye wanakuwa walipa kodi wakubwa na kuchangia maendeleo ya nchi.

Mwisho


No comments: