Tuesday, June 24, 2014

Utaratibu mpya kudhibiti msongamano wa magari Dar njiani kutangazwa

Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam

Katika kile kinachoonekana kama nia thabiti ya kuzuia tatizo sugu la msongamano wa magari katika jiji la Dar es Salaam, utaratibu mpya wa kudhibiti changamoto hiyo uko mbioni kutangazwa.

Mara utakapotangazwa, kila anayehusika hasa madereva katika jiji hilo kubwa la biashara watatakiwa kuuheshimu na kuufuata.

Akitangaza utaratibu huo mpya unaotarajiwa kuanza hivi karibuni, Afisa Mkuu Mtendaji wa Wakala wa Mabasiyaendayo Haraka (DART), Bi. Asteria Mlambo hatua hiyo inalenga kuondoa msongamano, kuimarisha usalama na usafi katika njia zote zilizokamilika za mradi wa mabasi hayo.

Mradi unaoendelea wa mabasi yaendayo haraka katika jiji la Dar es Salaam, unalenga kuimarisha huduma za usafiri na kuwa za kisasa zaidi pamoja na kupunguza msongamano ambao umekuwepo kwa kipindi kirefu sasa.

Katika awamu hii ya kwanza mradi huo unahusisha ujenzi wa barabara maalum ya umbali wa kilometa 20.9 kutoka Kimara hadi Kivukoni; barabara ya Msimbazi kuanzia Faya hadi eneo la Kariakoo-Gerezani na sehemu ya barabara ya Kawawa kuanzia Magomeni hadi njia panda ya Morocco.

“Tunatarajia utaratibu huu kuanza hivi karibuni,” Bi. Mlambo aliwaambia waandishi wa habari.

Akizungumzia mahitaji ya utaratibu huo mpya alisema gari zote zitakazotumia njia katika mfumo wa njia hizo mpya hazitatakiwa kuzidi mwendo wa kilometa 50 kwa saa hasa katika barabara ya Morogoro ambapo mradi huo unakaribia kukamilika.

Akielezea zaidi alisema magari hasa daladala hazitaruhusiwa kusimama njiani na pia itakuwa marufuku kufanya biashara ndogondogo au biashara ya aina yoyote katika maeneo ya njia hizo.

“Kwa sasa tunaangalia maeneo ya muda ambayo daladala zitaruhusiwa kusimama,” alisema na kuongeza kuwa taratibu zote zimekamilika na kuwa polisi wataanza kuhakikisha kuwa utaratibu huo unafuatwa hivi karibuni.

Kwa mujibu wa Afisa huyo wa DART, kupaki magari au kufanya biashara katika maeneo ya waenda kwa miguu haitaruhusiwa na watakaokiuka watakumbana na adhabu kali kwa mujibu wa taratibu.
Pamekuwa na mazoea ya madereva wa bajaji na pikipiki kupaki vyombo vyao katika njia za watembea kwa miguu.

“Napenda pia kuwataarifu wafanyabiashara kuacha kupaki magari ya mizigo katika njia kuu na kupakua au kupakia mizigo,” alisisitiza.
Aliongeza kuwa itakuwa marufuku pia kupaki magari katika njia za pembeni na wala pikipiki hazitaruhusiwa kupita katika njia za waenda kwa miguu.

“Makosa yatahusisha adhabu kali na faini ya pesa taslimu,” alisema.

Utaratibu huo utasimamiwa na kufuatiliwa na vyombo mbalimbali kama DART, askari wa usalama barabarani, Mamlaka ya Usafiri wa majini na nchi kavu (SUMATRA) pamoja na TANROADS.

Mwisho 


No comments: