Monday, June 16, 2014

Nia ya kuendeleza eneo huru bandari Mtwara yazidi kupata matumaini


Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Ukanda Maalumu wa Uwekezaji nchini (EPZA), Dk. Adelhelm Meru (wa pili kulia) akipokea hundi ya malipo ya awali ya Dola za kimarekani 526,280 kutoka kwa muwakilishi wa kampuni ya MAC Group Limited, Bw. Nagarayan Sankaranarayanan (wa pili kushoto) kwa ajili ya uendelezaji wa eneo huru la uwekezaji Bandari ya Mtwara jana jijini Dar es Salaam.  Kulia ni Mkurugenzi wa Uhamasishaji Uwekezaji wa Mamlaka hiyo, Bi. Zawadia Nanyaro (kulia) na Meneja biashara toka MAC Group, Bw. Kerioth Sanga.
 Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam

Moja ya makampuni manne yaliyofikia makubaliano na Mamlaka ya Ukanda Maalumu wa Uwekezaji nchini (EPZA) kwa ajili ya kutoa huduma mbalimbali kwa kampuni kubwa zinazofanya utafiti wa mafuta na gesi katika mkoa wa Mtwara imetoa malipo ya awali kwa ajili ya kufanikisha nia hiyo.

Kampuni hiyo, Altus Oilfield Services FPZ ya Singapore imetoa hundi ya dola za kimarekani 526, 280 sawa na Tshs 800 milioni kwa ajili ya kuanza ujenzi wa miundombinu ya eneo hilo.

Altus Oilfield Services FPZ inaundwa na kampuni ya Mac Group na Pacific International Lines.

Mkurugenzi Mkuu wa EPZA, Dr. Adelhelm Meru aliwaambia waandishi wa habari jana wakati wa kupokea hundi hiyo kuwa fedha hizo zitatumika kuanza kujenga miundombinu ya msingi kama barabara, umeme, maji na njia ya maji taka katika eneo la kampuni hiyo.

“Uwekezaji katika eneo hilo utasaidia kukuza ajira na uchumi wa nchi kuimarika zaidi,” alisema.
EPZA inaendeleza hekta 10 za eneo huru la bandari ya Mtwara.

Hekta hizo ni kati ya jumla ya hekta 110 za eneo hilo huru la bandari ambalo limetengwa na serikali kwa ajili ya uwekezaji mbalimbali.

Hekta hizo 10 zitaendelezwa kwa kuwekewa miundombinu inayotakiwa na kisha kugawiwa kwa makampuni ya kimataifa yanayofanya kazi za kutoa huduma mbalimbali kwa makampuni yanayofanya kazi ya utafiti wa mafuta na gesi katika mkoa wa Mtwara.

Kitakapomalizika, kituo hiki cha huduma kwa makampuni yanayofanya utafiti wa gesi na mafuta mkoani Mtwara kitakuwa cha kipekee si kwa Tanzania pekee bali katika ukanda mzima wa Mashariki na Kusini mwa Afrika.

Kampuni nyingine zilizoingia mkataba na EPZA mwezi uliopita kuwekeza katika eneo hilo ni Slumberger Seaco Inc ya Marekani, Tans Ocean Industries and Services LTD ya Dubai na Lenna ya Iran.

Zoezi la kupata wawekezaji katika eneo hili lilianza mwaka 2010 baada ya kampuni za utafutaji gesi na mafuta kuomba kuwepo kwa kampuni za watoa huduma.

Katika eneo hilo wawekezaji hao watajenga karakana kubwa kwa ajili ya kufanyia ukarabati na matengenezo ya vifaa vya ya mafuta na gesi.

Karakana hizo zitajengwa kisasa na zitakuwa na uwezo pia wa kuhudumia nchi jirani kama Kenya, Msumbiji, na Afrika Kusini.

Muwakilishi wa kampuni ya MAC Group Limited aliyekabidhi hundi hiyo, Bw. Nagarayan Sankaranarayanan alisema kampuni yake imejiandaa kuanza kufanya kazi ya kutoa huduma kwa makampuni ya utafutaji gesi na mafuta.

“Tumejipanga kutoa huduma bora kama ilivyokusuudiwa,”alisema.

Mwisho



No comments: