Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Mamlaka ya Ukanda Maalumu wa Uwekezaji nchini (EPZA) imesaini
makubaliano na Benki ya Maendeleo
Tanzania (TIB) kwa ajili ya kupata mikopo ya kujenga miundombinu itakayovutia
wawekezaji kuanzisha viwanda katika maeneo yake maalumu.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo, Dkt. Adelhelm Meru aliwaambia waandishi
wa habari mara baada ya kusaini mkataba huo, kuwa makubaliano hayo yanalenga
kuendeleza maeneo ya mamlaka hiyo yaliyosambaa pote nchini.
“Makubaliano haya ni muhimu sana kwa maendeleo ya nchi yetu,” Dk. Meru
aliwaambia waandishi wa habari jana.
Alisema kupitia makubaliano hayo maeneo maalumu ya uwekezaji kama
Bagamoyo, Mtwara, Kigoma, Tanga na mengine yote yaliyo katika mikoa 20 yatapata
miundombinu itakayovutia wawekezaji wa ndani na nje.
Alisema makubariano hayo yanalenga kutimiza ndoto ya muda mrefu ya
kujenga miundombinu katika maeneo hayo.
“Hii ni dalili nzuri kwa vile kwa sasa badala ya kuomba fedha mfuko wa serikali
au kutoka nje ya nchi, sasa nchi yetu ina benki yenye uwezo wa kugharimia
miradi mbalimbali,”alisema Dkt. Meru.
Alifafanua kwamba wawekezaji wanapenda kuwekeza katika maeneo ambayo
tayari yana miundombinu na hivyo kwa kuchukua hatua hiyo wengi watavutiwa na
maeneo hayo na kuiletea nchi faida.
Aliongeza kusema kuwa viwanda vikianzishwa katika maeneo hayo watanzania
wengi watapata ajira, mapato yataongezeka na uchumi wa nchi utaimarika zaidi.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Bw. Peter Noni alisema benki
yake tayari imejenga uwezo wa kifedha wa kutosha kwa ajili ya kusaidia miradi
ya ujenzi ya miundombinu itakayovutia wawekezaji kujenga viwanda.
“Tunatambua maeneo maalumu ya mamlaka hii ni ya kitaifa na yanahitaji
kuendelezwa kuvutia uwekezaji, ni wajibu wetu kutekeleza jambo hili,”alisema.
Alisema Wizara ya Nishati na Madini inatarajia kuongeza uzalishaji wa
umeme kufikia Megawati 3,000 baada ya mwaka mmoja, na hivyo ni vyema kuwa na
miundombinu inayovutia uwekezaji kuja kujenga viwanda nchini.
“Kwa muda mrefu tumekuwa hatuna viwanda vingi kutokana na umeme kutokuwa
na uhakika, sasa uhakika huu upo,” alisema, na kuongeza kuwa mkataba huo ni
moja ya matayarisho hayo.
Alisema benki hiyo imeamua kushirikiana na mamlaka hiyo kwa vile tayari
ina maeneo maalumu na ni vyema yaandaliwe mapema kwa kujengwa miundombinu
inayotakiwa na wawekezaji.
Mwisho
No comments:
Post a Comment