Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF), Bw.
Godfrey Simbeye (kushoto) akisisitiza jambo kwa Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya
Waziri Mkuu, TAMISEMI, Bw. Kagyabukama Kiliba wakati wa warsha ya kujadili
ripoti ya mshauri mwelekezi kuhusu uboreshaji utoaji wa vibali vya ujenzi hapa
nchini jana jijini Dar es Salaam. Warsha hiyo inayomalizika leo
imetayarishwa na TPSF.
Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Taasisi ya Sekta Binafsi nchini (TPSF) imesema Tanzania haiwezi
kuendelea kukwamishwa na urasimu wa utoaji wa vibali vya ujenzi ambavyo
vinarudisha nyuma juhudi za kujenga mazingira bora ya kufanya biashara na
kuvutia uwekezaji.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF), Bw. Godfrey
Simbeye amesema hivyo jana wakati wa warsha ya kujadili ripoti ya mshauri
mwelekezi kuhusu uboreshaji utoaji wa vibali vya ujenzi hapa nchini.
“Suala la utoaji vibali vya ujenzi limekumbwa na changamoto ya urasimu
ambao unachelewesha kupata vibali vya ujenzi na kusababisha hasara kwa sekta
binafsi na kwa taifa,”alisema jana jijini Dar es Salaam.
Alisema ili nchi iweze kuondokana na changamoto hiyo inahitaji kuboresha
mazingira ya usimamizi wa ardhi pamoja na utoaji wa vibali vya ujenzi.
Kwa sasa juhudi kubwa zinafanyika kuvutia wawekezaji wa ndani na nje
lakini wanapokuwa tayari kujenga wanachukua miaka mingi kupata kibali cha
ujenzi.
Alisema ucheleweshaji huo pia unasababisha kupoteza ajira, na fursa ya
kutumia majengo yaliyokusudiwa kujegwa kama njia ya kuleta maendeleo.
Akitoa mfano alisema nchi jirani ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki
zimepiga hatua kubwa katika utoaji vibali hivyo kwa njia ya mtandao.
“Ni lazima tubadilike, wawekezaji tunaovutia ni hao hao,” alisema.
Alisema mpango elekezi wa kuboresha mazingira ya biashara unaosimiwa na
Ofisi ya waziri Mkuu uliainisha upatakanaji wa vibali vya ujenzi kama eneo
linalohitaji kuboreshwa na kuundiwa kikosi kazi cha serikali ambacho
kilishirikisha sekta binafsi.
Kwa kutambua hilo sekta binafsi iliamua kuunda kikosi kazi chake ambacho
kilikuwa kinafuatilia utekelezaji wa maboresho yaliyoainishwa kwenye mpango huo
na kilifanya tafiti ya changamoto ya upatakanaji wa vibali hivyo.
“Kikosi kazi hiki kimekuja na ripoti ambayo tunaijadili hapa na tutatoa
mapendekezo ya jisni ya kuzipunguza changamoto za ucheleweshaji utoaji
vibali,”alisema.
Mkutano huo unamalizika leo.
Alisema mapendekezo hayo baada ya kutolewa yatapelekwa serikali ili
waweze kuyafanyia kazi na kuiondosha changamoto hiyo na changamto zingine
ambazo nchi haifanyi vizuri kulingana na ripoti ya dunia inayotolewa kila
mwaka.
Awali, Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI, Bw.
Kagyabukama Kiliba alisema hatua ya sekta binafsi kuandaa ripoti na kuijadili
ni hatua ya msingi katika kujenga ushirikiano na serikali katika kutafuta
ufumbuzi wa changamoto za kuboresha uwekezaji.
“Nawahakikishia sisi kama serikali tutayachukua mapendekezo yenu na
kwenda kuyafanyia kazi kwa nia ya kuzidi kujenga mazingiara bora ya utoaji
vibali vya ujenzi,”alisema.
Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI, ndiyo inayohusika na utekelezaji wa
mpango elekezi wa kuboresha mazingira ya biashara katika kiashiria cha vibali
vya ujenzi.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Tanzania Civil Engineering Contractors
Association (TACECA), Bw. Clement Mworia alisema utoji wa vibali umekuwa ni
tatizo kubwa katika sekta ndogo ya ujenzi na hiyo inarudisha nyuma maendeleo
yake.
“Kumekuwepo na hali ya kuporomoka kwa majengo hapa nchini hasa Dar es
Salaam, hii inasabishwa na urasimu wa utoaji vibali ambapo watu wanajenga bila
ya halmashauri kukagua msingi wa ujenzi,”alisema.
Warsha hiyo inashirikisha wajumbe toka
sekta binafsi na umma.
Mwisho.