Mkurugenzi wa Taasisi ya Uthamini
Raslimali (IRA) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Prof. Amos Majule (second
right) akisisitiza jambo kwa waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam
alipokuwa anatangaza mkutano mkubwa wa wanasayansi utakaofanyika kuanzia tarehe
27 mwezi huu Dar es Salaam. Wengine pia
wajumbe wa kamati ya maandalizi, Dk. Catherine Masao (kulia), Dk. Stephanie
Duvail (pili kushoto) na Bw. Pellage Kauzeni (kushoto).
Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Jiji la Dar es Salaam linatarajiwa kuwa mwenyeji wa kongamano
kubwa la wanasayansi kutoka bara la Afrika na nje ya bara hilo wiki ijayo
kuongelea mabadiliko yanayotokea sasa katika maeneo ya ardhi oevu na makutano
ya mito na bahari.
Akitangaza mkutano huo jijini Dar es Salaam jana, mmoja wa
wajumbe wa kamati ya maandalizi, Prof. Amos Majule alisema kongamano hilo
litakalojulikana kama Afrideltas litafanyika kuanzia tarehe 27-30 May 2014.
Prof. Majule ambaye pia ni Mkurugenzi wa Taasisi ya Uthamini
Raslimali (IRA) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) alitoa wito kwa wadau
mbalimbali wanaotaka kuhudhuria mkutano huo wa kihistoria kuhakikisha
wanajisajili kwa wakati.
Prof. Majule alieleza kuwa kongamano hilo litahusisha
wataalamu wa nje na ndani watakaoangalia na kufahamu zaidi faida zinazopatikana
katika maeneo hayo ya ardhioevu na yale maeneo ambayo mto unakutana na bahari.
Alisema mkutano huo pia utapata taarifa mbalimbali za utafiti
kutoka nchi nyingine kuhusu maeneo hayo na kubadilishana uzoefu baina ya
wataalamu hao.
“Natoa wito kwa wadau wanaopenda kuhudhuria mkutano huu
kujisajili mapema,” alisema, na kushauri kutembelea tovuti ya www.kenweb.or.ke au
kuwasiliana na taasisi ya IRA kwa taarifa zaidi.
Mtaalamu huyo alisema kuna mabadiliko mengi yanayotokea sasa
katika maeneo hayo kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa na shughuli za
binadamu na hayo yote yanatarajiwa kuangaliwa kwa kina katika kongamano hilo na
kuja na maazimio kwa siku zijazo.
Mjumbe mwingine wa kamati ya maandalizi, Dk. Catherine Masao
alisema maeneo hayo ni uhimu sana kwa kuwa binadamu wanayategemea kwa maisha
yao.
“Maeneo haya yanasaidia na kubeba uhai wa wanyama na mimea,”
alisema, na kuongeza kuwa pia maeneo ya ardhioevu yanasaidia katika kurekebisha
athari za uchafuzi wa mazingira unaofanywa na binadamu.
Akielezea jinsi mabadiliko ya maeneo ya ardhioevu
yanavyoathiri maisha ya watu katika bara la Afrika, mjumbe mwingine wa kamati
hiyo, Dk. Stephanie Duvail alisema ujenzi wa mabwawa katika ukanda wa juu wa
mto unaweza kusababisha mabadiliko na katika ardhioevu na kuathiri maisha ya
watu.
Akitoa mfano, Bw. Pellage Kauzeni toka Wizara ya Maliasili na
Utalii alisema bonde la Kilombero ni moja ya maeneo ya ardhioevu hapa nchini
ambayo shughuli za kibinadamu zinapelekea mabadiliko kwa kiwango kikubwa katika
eneo hilo.
Katika siku ya tatu ya mkutano huo, inatarajiwa kuwa
wanasayansi wataungana na watunga sera na wadau wengine toka serikalini akiwemo
Waziri wa Maliasili na Utalii, Bw. Lazaro Nyalandu ambae atafunga mkutano ili
kujadiliana kuhusu majumuisho na hatua za kuchukua ili kulinda maeneo hayo.
Mwisho.