Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji nchini (TIC), Bi. Juliet
Kairuki (kushoto) akifafanua jambo wakati wa ziara ya Gavana wa kisiwa cha Anjouan Bw. Anissi Chamsidine katika
kituo hicho jana jijini Dar es Salaam.
Gavana huyo yuko nchini kwa ziara ya wiki moja. Katikati ni mke wa Gavana huyo, Bi. Laouya
Shamsidine.
Mkurugenzi
Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji nchini (TIC) Bi. Juliet Kairuki (katikati) akimkabidhi
zawadi ya picha Gavana wa kisiwa cha Anjouan Bw. Anissi
Chamsidine (kulia) ambaye yupo nchini kwa ziara ya wiki moja. Gavana huyo alitembelea kituo hicho
jana. Kushoto ni mke wa Gavana, Bi. Laouya
Shamsidine.
Na
Mwandishi wetu, Dar es Salaam.
Watanzania
wametakiwa kuchangamkia fursa za uwekezaji zinazopatikana katika kisiwa cha
Anjouan nchini Comoro ili kukuza na kuendeleza ushirikiano uliopo kwa maslahi
ya kijamii na kiuchumi kati ya pande hizo mbili.
Gavana
wa Anjouan, Bw Anissi Chamsidine alieleza hayo alipotembelea Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) jana jijini Dar es Salaam.
“Tuna fursa nyingi za uwekezaji katika kisiwa cha
Anjouan na tunaamini watanzania wako katika nafasi nzuri ya kuzitumia,” alisema
na kuongeza kuwa ushirikiano kati ya pande hizo mbili ni wa damu na wa
kihistoria.
Alisema kuwa kuna unmuhimu wa kuendelea
kushirikiana katika eneo la uwekezaji na kutaja maeneo ambayo yanahitaji
uwekezaji kuwa ni elimu, utalii, nishati na katika sekta ya afya.
“Tuna hospitali kubwa zinajengwa lakini tatizo ni
kukosekana kwa wataalamu wa afya ikiwemo wauguzi na madaktari hivyo tunaomba
watanzania waje kutusaidia katika eneo hilo,” alisema.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa TIC, Bi. Juliet Kairuki
amesema kuwa ujio wa Gavana huyo na ujumbe wa wawekezaji utasaidia kufungua
fursa za uwekezaji na ushirikiano mzuri kiuchumi kati ya nchi hizo.
“TIC na serikali inathamini ziara ya Gavana na
ujumbe wake, mahusiano yetu ni ya siku nyingi na tungependa kuyaimarisha,”
alisema na kuongeza kuwa ziara hiyo itasaidia kuvutia uwekezaji kutoka katika
kisiwa hicho.
Kama moja ya ratiba zake akiwa hapa nchini,
Gavana huyo anatarajiwa kushiriki katika kongamano kubwa la uwekezaji kanda ya
kaskazini linalotarajiwa kuanza mkoani Tanga asubuhi hii.
Benki mbalimbali, Bodi ya Utalii Tanzania
(TTB), Mamlaka ya Uwekezaji Tanzania (EPZA) na Muungano wa wenye viwanda
Tanzania (CTI) ni baadhi ya walioalikwa kwenye kongamano hilo.
Kongamano hilo linatarajia kuvutia washiriki
1,500 toka ndani na nje ya nchi, ikiwemo China.
Baadhi ya vivutio katika kanda ya kaskazini ni
ardhi yenye rutuba kwa kilimo cha mazao ya biashara, mbogamboga na matunda,
madini, na utalii.
Gavana huyo atakutana pia na wakuu wa mikoa
inayounda kanda hiyo ya kaskazini, mmoja mmoja wakati wa kongamano hilo.
Mratibu wa ziara hiyo kwa upande wa Anjouan,
Bw. Allaoui Toihirdine alisema kuwa mahusiano ya Anjouan na Tanzania ni ya
kihistoria na kwamba ziara hiyo itaimarisha uhusiano huo.
Alisema, Anjouan inatambua mchango mkubwa
uliotolewa na Tanzania katika kukikomboa kisiwa hicho mwaka 2009 na kukirudisha
katika utawala wa muungano wa visiwa vya Comoro.
Mwisho
No comments:
Post a Comment