Naibu Waziri, Wizara ya Mawasiliano,
Sayansi na Teknolojia, Bw. Januari Makamba (kushoto) akimsikiliza Mratibu wa
Mauzo wa Kampuni ya Mawasiliano Tanzania (TTCL) Bw. Thomasi Lemunge katika
banda la kampuni hiyo wakati wa kongamano la kimataifa la mawasiliano lililomalizika
jana jijini Dar es Salaam. Kushoto kwa Waziri ni Afisa Mtendaji Mkuu wa TTCL, Dkt.
Kamugisha Kazaura.
Naibu Waziri, Wizara ya Mawasiliano,
Sayansi na Teknolojia, Bw. Januari Makamba (kushoto) akimsikiliza Afisa
Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Mawasiliano Tanzania (TTCL), Dkt. Kamugisha Kazaura
alipotembelea banda la kampuni hiyo wakati wa kongamano la kimataifa la
mawasiliano lililomalizika jana jijini Dar es Salaam.
Naibu
Waziri, Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Bw. Januari Makamba akizungumza
na Mkurugenzi wa Kampuni ya Mawasiliano ya Kijapan, Bw. Norifumi Egi (katikati)
na Bw. Victor Pitamber wa Business Development Internet Solution, baada ya
kutembelea banda lao wakati wa kongamano la kimataifa la mawasiliano
lililomalizika jana jijini Dar es Salaam.
Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Wawekezaji wa ndani na nje ya nchi
wameshauriwa kutumia fursa zilizopo katika sekta ya mawasiliano na maeneo
mengine nchini kuja kuwekeza kwa faida ya pande zote mbili.
Naibu waziri wa wizara ya Mawasiliano,
Sayansi na Teknolojia, Bw. Januari Makamba aliwaambia waandishi wa habari jana
katika kongamano la kimataifa la wadau wa mawasiliano kuwa Tanzania ina fursa
nyingi za uwekezaji.
“Tuna fursa nyingi na mazingira ya
uwekezaji ni mazuri na yanazidi kuboreshwa,” alisema.
Akitoa mfano alisema serikali imetumia
fedha nyingi kujenga mkongo wa taifa wa mawasiliano ambao kwa sasa umefungua
milango kwa sekta ya mawasiliano kwa Tanzania na nchi za jirani.
“Mkongo huu ulijengwa kwa ajili ya taifa
letu, lakini pia umefungua njia mpya kwa mataifa mengine yakiwemo ya Afrika
Mashariki, Kati na Kusini kutumia kwa mapatano ya kibiashara,” alisema.
Alisistiza kwamba makampuni yanayotaka
kutumia mkongo wa taifa kufikisha huduma za mawasiliano katika nchi mbalimbali
yanakaribishwa ili kufikia lengo na kupanua wigo wa mawasiliano
katika bara hili na kufikia maendeleo.
Mkongo wa taifa wa mawasiliano ni
muundombinu wa teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA) unaojengwa na
serikali kupitia wizara ya mawasiliano, Sayansi na Teknolojia na kusimamiwa na
kuendeshwa na TTCL.
Tayari baadhi ya makampuni ya mawasiliano
ya nchi jirani yameshaunganishwa kupitia Tanzania na nchi zaidi kama Uganda na
Msumbiji zinaendelea kuzungumza na serikali kuona jinsi ya kujiunga nao.
Ujenzi wa mkongo wa taifa wa mawasiliano
unaendelea kujengwa kwa awamu na ukikamilika utakua na urefu wa zaidi ya
kilomita 10,000.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni
ya Mawasiliano Tanzania (TTCL), Dkt. Kamugisha Kazaura alisema mkutano huo wa
wadau wa mawasiliano ulitoa fursa za kibiashara ambapo waliweza kubadilishana
mawazo, na kujifunza.
“Tumefikia makubaliano ya kibiashara kati
ya kampuni yetu na makampuni ya watoa huduma yaliyoshiriki katika mkutano
huu...lengo ni kupata wateja wengi wa mkongo wa taifa,” alisema.
Alisema kwa sasa kuna mikongo mitatu
inayopita baharini hivyo mataifa hayo na makampuni za watoa huduma za
mawasiliano yatumie fursa na kunganishwa na mikongo huo wa taifa.
Afisa Mtendaji Mkuu wa kampuni ya
kimataifa ya LIQUID TELECOM yenye makao makuu nchini Mauritius, Bw. Hans
Haerdtle, alisema kampuni yao ilifaidika na mkutano huo kwa kubadilishana
mawazo na kujifunza kutoka kwa wadau wengine wa mawasiliano.
“Huu ni mkutano muhimu kwetu tumejifunza
mengi, na tumeweza kutumia fursa hii kufanya mazungumzo ya kibiashara na
makampuni mbalimbali ikiwemo TTCL,”alisema.
Alisema kampuni yao imejidhatiti kuzidi
kupanua na kutoa huduma bora kwa kuwekeza zaidi ili kutoa huduma bora kwa
wateja wake katika eneo la Afrika Mashariki, kati na kusini.
Mkutano huo uliwaleta pamoja watoa huduma
za mawasiliano 460 kampuni kama ya TTCL, wauza vifaa vya mawasiliano, kampuni
zinazotoa huduma za mawasiliano kwa njia ya satelaiti na mikongo ya
baharini.
Mwisho
No comments:
Post a Comment