Kaimu Mwenyekiti wa jopo la makamu wakuu wa vyuo vikuu na
wakuu wa vyuo Tanzania (CVCPT) na Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe,
Taaluma, Prof. Josephat Itika (kushoto) akizungumza na Waziri wa Elimu na
Mafunzo ya Vitendo, Dkt. Shukuru Kawambwa aliyekuwa mgeni rasmi wakati wa
kongamano la tano la elimu ya juu jijini Arusha jana. Katikati ni Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu
Mzumbe, Utawalana Fedha, Prof. Faustin Kamuzora.
Kaimu
Mwenyekiti wa jopo la makamu wakuu wa vyuo vikuu na wakuu wa vyuo Tanzania
(CVCPT) na Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Taaluma, Prof. Josephat
Itika (kushoto) akimpatia zawadi Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Vitendo, Dkt.
Shukuru Kawambwa aliyekuwa mgeni rasmi wakati wa kongamano la tano la elimu ya
juu jijini Arusha jana.
Na Mwandishi
wetu, Arusha
Serikali imesema kwamba iko tayari kutoa ushirikiano zaidi
wa mikakati itakayoanzishwa kupanua wigo wa mahusiano kati ya vyuo vya elimu ya
juu kwa upande mmoja na waajiri ikiwemo makampuni na viwanda kwa upande
mwingine kuongeza thamani ya elimu hapa nchini.
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Vitendo, Dkt. Shukuru
Kawambwa amesema hayo alipokua akifungua kongamano la tano la elimu ya juu
jijini Arusha jana.
Mada kuu ya mkutano wa mwaka huu uliotayarishwa na jopo la
makamu wakuu wa vyuo vikuu na wakuu wa vyuo Tanzania (CVCPT) ni jinsi gani vyuo
vikuu vinaweza kushirikiana na waajiri ikiwemo viwanda na makampuni ili kujenga
elimu ya juu endelevu Tanzania.
Waziri alisema kuwa serikali kupitia wizara yake
itahakikisha inafanyia kazi na kufuatilia mapendekezo yatakayotokana na
kongamano hilo la siku mbili.
“Ninataraji kuwa CVCPT na wadau wengine watashirikiana na
wizara yangu kuhakikisha mapendekezo ya kongamano hili yanakua yenye manufaa
kwa nchi yetu,” alisema.
Alisema wizara yake kupitia programu mbalimbali
inazingatia na kutambua umuhimu wa makampuni na viwanda katika kuendeleza
elimu.
Alitoa wito kwa CVCPT kuhakikisha inaendeleza makongamano
kama haya ili kuifanya elimu nchini kuwa ya thamani na endelevu.
“Ninatoa wito pia kwa wakuu wasaidizi wa vyuo vikuu nchini
kuhudhuria kwa wingi katika makongamano mengine siku zijazo,” alisema.
Katibu Mtendaji wa sekretarieti ya Vyuo Vikuu Afrika
Mashariki (IUCEA), Prof. Mayunga Nkunya alisema kwamba chombo hicho kinaunga
mkono ushirikiano kati ya vyuo vikuu na sekta binafsi.
Alisema IUCEA iko katika mikakati mbalimbali kufanikisha
hilo kama kushiriki majadiliano ya kuimarisha mitaala, na kuongeza mahusiano na
sekta binafsi katika tafiti na ubunifu.
Mkurugenzi wa Idara ya Elimu ya Juu katika Wizara ya Elimu
na Mafunzo ya Vitendo, Prof. Sylvia Temu alisema ushirikiano kati ya vyuo vikuu
na waajiri lazima uanzie katika ngazi za juu vyuoni.
“Muda sasa umefika kwa makamu wakuu wa vyuo kutenga muda
na kuwa na wadau katika viwanda na makampuni ili kuona jinsi ya kufanya kazi
pamoja,” alisema.
Alisema Wizara inaunga mkono ushirika wa aina hiyo maana
ndio unaochochea matumizi bora na yenye tija ya utaalamu na elimu.
Kaimu Mwenyekiti wa CVCPT, Prof. Josephat Itika alishukuru
wafadhili waliofanikisha kongamano hilo wakiwepo Tume ya Vyuo Vikuu nchini
(TCU), Tanzania Investment Bank (TIB) na Tume ya
Mawasiliano Tanzania (TCRA).
“Tunawahakikishia kuwa tutafanyia kazi mchango wao na
kuleta ufanisi kama inavyotakiwa,” alisema.
Lengo kubwa la CVCPT ni kukutanisha wadau wa elimu ya juu
kwa upande mmoja na wadau wengine wa maendeleo nchini kwa lengo la kujadiliana
jinsi ya kuimarisha elimu ya juu na raslimali watu hapa nchini.
CVCPT ilianzishwa mwaka 2005.
Wajumbe wa CVCPT ni makamu wakuu wa vyuo vikuu pamoja na
wakuu wa taasisi za elimu binafsi na vya umma pamoja na katibu mtendaji wa TCU.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment