Na Mwandishi wetu, Tanga
Uhusianao kati ya Anjouan, moja ya visiwa vinavyounda nchi ya
Comoro na Tanzania unazidi kuimarika baada ya pande hizo kutiliana saini
mkataba wa ushirikiano katika maswala ya uwekezaji na biashara kwa faida ya
wananchi wao.
Makubaliano hayo yametiwa saini kati ya Anjouan kwa upande
mmoja na mikoa minne inayounda kanda ya kaskazini ambayo ni Tanga, Kilimanjaro,
Arusha na Manyara wakati wa kongamano la uwekezaji mwishoni mwa wiki mjini
Tanga.
Gavana wa Kisiwa cha Anjouan, Bw. Anissi Chamsidine, alitia
saini kwa niaba ya watu wake wakati mikoa hiyo minne iliwakilishwa na Makatibu
Tawala wa mikoa hiyo.
Akiongea muda mfupi kabla hajatia saini yake, Gavana Chamsidine
aliwaambia washiriki wa kongamano kuwa kisiwa chake kina soko kubwa la vitu
kutoka Tanzania.
“Leteni bidhaa mbalimbali kama mbogamboga, nyama na
nyinginezo,” aliwaambia wajumbe hao wa kongamano lililotayarishwa na kituo cha
uwekezaji Tanzania (TIC).
Alisema kisiwa chake kina fursa kama za utalii, afya, na
elimu ambazo zinahitaji kuendelezwa na kukaribisha watu kuangalia nafasi hizo
za kiuchumi kwa faida ya pande zote mbili.
Gavana huyo pamoja na ujumbe wake walihudhuria kongamano hilo
kama moja ya ratiba katika ziara yao kuangalia fursa za uwekezaji na biashara
hapa nchini.
Wakati wa kongamano hilo, Gavana na
ujumbe wake walikutana na wakuu wote wa mikoa, TIC, na maafisa wengine wa
serikali kuainisha maeneo ya ushirikiano na namna nzuri ya kushirikiana kwa faida
ya pande zote mbili.
Akifunga kongamano hilo, Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwezeshaji na Uwekezaji, Dkt. Mary Nagu aliwataka
wakuu wa mikoa, wilaya na wakurugenzi wa wilaya kufungua vituo vya kusaidia
maswala ya uwekezaji katika maeneo yao ambavyo vitaratibiwa na TIC.
“Vituo hivyo vilenge kupunguza
gharama za kufanya biashara hapa nchini,” alisema.
Alifafanua kuwa gharama ya kufanya
biashara hapa nchini bado ni kubwa ikilinganishwa na nchini nyingine za Afrika
Mashariki na kwamba hilo lazima lifanyiwe kazi ili kuvutia zaidi mitaji na
kuleta maendeleo ya haraka.
Alisema ni wakati muafaka sasa kwa
kila mkoa kujiwekea malengo yatakayopimwa kila mwaka kuangalia uwekezaji
ulioingia katika mkoa husika, changamoto na nini kifanyike kuvutia zaidi uwekezaji.
“Kipimo cha kwanza cha mkakati huo
itakua kuangalia idadi ya miradi ya uwekezaji katika mkoa,” alisema.
Alisema katika mkakati huo kila mkoa
utatakiwa kuonyesha mipango inayotarajiwa kufanyika katika kipindi fulani.
“TIC itatengeneza ripoti moja kwa
ajili ya ufuatiliaji zaidi na utekelezaji kupitia ofisi yangu,” alisema.
Kongamano hilo la siku mbili
lililofunguliwa na waziri mkuu Mizengo Pinda lilihudhuriwa na wawekezaji zaidi
ya 1,500 toka ndani na nje ya nchi pamoja na maafisa wengine toka sekta binafsi
na umma, viongozi wa dini, mabalozi na wadau wengine wa mandeleo.
Mwisho
No comments:
Post a Comment