Monday, September 23, 2013

Gavana wa Anjouan kuwasili leo, kushiriki mkutano wa uwekezaji Alhamis

Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Gavana wa kisiwa cha Anjouan, moja ya visiwa vinavyounda nchi ya Comoro, Anissi Chamsidine anatarajiwa kufika Tanzania leo kuanza ziara yake ya wiki moja.
Akiwa hapa nchini, Gavana huyo anatarajia kukutana na viongozi mbalimbali wa serikali na jumuia ya wafanyabiashara kutoka sekta mbalimbali za uchumi.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Gavana Chamsidine pia atashiriki katika kongamano kubwa la uwekezaji kwa mikoa ya kanda ya Kaskazini litakalofanyika mkoani Tanga kuanzia Alhamis wiki hii.
Kongamano hilo linatarajia kuvutia wawekezaji wa ndani na nje kujionea fursa katika kanda hiyo.  Mikoa inayounda kanda ya kaskazini ni pamoja na Tanga, Kilimanjaro, Manyara na Arusha.
Ziara ya Gavana wa kisiwa hicho inaratibiwa na TIC kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.
“Siku ya Jumanne, Gavana atakutana na wawakilishi wa kampuni mbalimbali katika ofisi za TIC na kuangalia fursa za uwekezaji na maeneo ya ushirikiano,” ilisema taarifa hiyo iliyotiwa saini na Mkurugenzi Mtendaji wa kituo hicho, Bi. Juliet Kairuki.
Bi. Kairuki amesema kuwa TIC na serikali inathamini ziara ya Gavana huyo na ujumbe wake na kwamba Tanzania ina mahusiano makubwa ya kiuchumi na kijamii na kisiwa cha Anjouan.
“Ziara hii itasaidia kuvutia uwekezaji kutoka katika kisiwa hiki na sehemu nyingine duniani,” alisema katika taarifa yake.
Benki mbalimbali, Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Mamlaka ya Uwekezaji Tanzania (EPZA) na Muungano wa wenye viwanda Tanzania (CTI) ni baadhi ya walioalikwa kwenye kongamano hilo.
Kongamano hilo linatarajia kuvutia washiriki 1,500 toka ndani na nje ya nchi, ikiwemo China.Gavana huyo pia atafanya mazungumzo na kila Mkuu wa Mkoa husika kwenye kongomano la uwekezaji.
Mkoa wa Tanga unapanua bandari yake na kuifanya kuwa ya kisasa zaidi, jambo ambalo linatazamiwa kuvutia na kufaidisha zaidi wawekezaji katika kanda hiyo.
Baadhi ya vivutio katika kanda ya kaskazini ni ardhi yenye rutuba kwa kilimo cha mazao ya biashara, mbogamboga na matunda, madini, na utalii.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Gavana huyo atakutana pia na wakuu wa mikoa inayounda kanda hiyo ya kaskazini, mmoja mmoja wakati wa kongamano hilo.
Akiongea na waandishi wa habari wiki iliyopita jijini Dar es Salaam, mratibu wa ziara hiyo kwa upande wa Anjouan, Bw. Allaoui Toihirdine alisema kuwa mahusiano ya Anjouan na Tanzania ni ya kihistoria na kwamba ziara hiyo itaimarisha uhusiano huo.
Alisema, Anjouan inatambua mchango mkubwa uliotolewa na Tanzania katika kukikomboa kisiwa hicho mwaka 2009 na kukirudisha katika utawala wa muungano wa visiwa vya Comoro.
Mwisho

No comments: