Thursday, September 19, 2013

Mkongo wa mawasiliano wa Taifa wakubalika zaidi

Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam

Katika kile kinachoonyesha kufanikiwa kwa mkongo wa taifa wa mawasiliano, nchi nyingi zaidi zinaendelea kufanya mazungumzo na Tanzania ili kuunganishwa nao.

Kwa sasa nchi za Uganda na Msumbiji zinaendelea kufanya mazungumza na Tanzania huku  baadhi ya kampuni kutoka Kenya zikisaini makubaliano ya kuutumia.

Mkuu wa Masoko na Mauzo wa Kampuni ya Mawasiliano Tanzania (TTCL), Bw. Peter Ngota aliwambia waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam wakati wa mkutano wa kujenga uwezo wa  mawasiliano Afrika kuwa jambo hilo ni la kutia moyo kwa nchi.
“Kwa kweli tuipongeze Serikali kwa kujenga mkongo huu ambao unasifiwa na wadau wengi wa mawasiliano umejengwa kitaalamu  na imara,” alisema na kuongeza kuwa wadau wa mkutano huo toka nchi mbalimbali wameonyesha kuvutiwa na mkongo huo.

Tanzania imeunganishwa na mikongo ya baharini Afrika Mashariki ikiwemo ya SEACOM, EASSY na SEAS ambayo imesaidia kujenga uwezo mkubwa wa ufanisi katika mawasiliano.

Alisema nchi za Afrika zinataka kutumia fursa ya mikongo iliyopo Afrika ikiwemo ya Afrika Mshariki na Magharibi kujenga kituo cha internet cha Afrika kwa ajili ya kusambaza mwasiliano katika bara hilo bila kupitia Ulaya.

Alisema mkongo wa Taifa umesifiwa na mkutano mkuu wa wadau wa Mawasiliano duniani kuwa umejengwa kitaalamu na unavutia wawekezaji wengi kutafua fursa za kuwekeza katika sekta ya mawasiliano katika Ukanda wa Afrika Masharika, kati, na Kusini.
“Kwa sasa ukitumia internet inatumia miundombinu ya Ulaya na lazima mawaslinano hayo yafike huko, lakini baada ya kujenga miundombinu yetu hayatafika huko na hiyo itakuwa ni hatua kubwa katika mawasiliano katika bara hili,” alisisitiza.

Mkurugenzi Mtendaji wa wa VODAFONE  Ghana, Julius Nkansah Owusu Kyerematen alisema wakati umefika kwa Afrika Kutumia mikongo kuboresha mawasiliano kwa ajili ya kuchochea maendeleo.

“Nchi zetu hizi bado zipo katika safari ndefu kiuchumi hivyo ni vema kuhakikisha huduma za mawasiliano zinaboreshwa katika nchi zote ili kufikia malengo ya bara hili,” alisema.
Alisema nchi zisizo kuwa na mikongo zifanye jitihada ya kujiunga na mikongo hiyo ili kuhakikisha mawasiliano yanapatikana kwa ajili ya kuchoche utoaji huduma mbalimbali zikiwemo za elimu na afya.
Mkuu wa Idara ya Mkongo wa Taifa (TTCL), Bw. Adin Mgendi alisema mkutano huo utasaidia kujenga mahusiano ya kibiashara na kuimarisha mahusiano yaliyokuwepo na kuangalia fursa mpya.

“Hii ni fursa tuliyoipata kujifunza toka kwa wenzetu kama Ghana na Angola ambao wana mikongo,” alisema.
Alisema mikongo ya Afrika ina nafasi kubwa ya kuliendeleza bara hili kufikia malengo yake kiuchumi.

Mkutano huo uliomalizika jana umehudhuriwa na makampuni 460 kutoka Afrika na nje ya Afrika ambao ni wawekezaji na waendeshaji wa miundombinu ya mawasiliano.


Mwisho  

No comments: