Sunday, September 15, 2013

Dkt. Turuka: Serikali kuendelea kuboresha mazingira ya biashara, uwekezaji




Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Dtk Florens Turuka akielezea nia ya serilakali kuendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara hapa nchini kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) jijini Dar es Salaam mwishoni mwa juma.
 


Na Mwandishi wetu
Serikali imewahakikishia wawekezaji kuwa itaendelea kuweka mazingira bora  ya kufanya biashara na uwekezaji kama chachu ya  kuvutia zaidi uwekezaji  hapa nchini ilikuongeza kasi ya maendeleo na ukuaji  wa uchumi.
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Dkt. Florens Turuka aliwaambia waandishi wa habari mwishoni mwa wiki kuwa mazingira ya uwekezaji nchini yatasaidia kuvutia wawekezaji katika sekta mbalimbali za kiuchumi na huduma.
“Serikali imeboresha mazingira ya uwekezaji kwa kuweka sera na sheria” ambazo zinatoa fursa kwa wawekezaji kufanya shughuli zao bila vikwazo vyovyote hapa nchini,” alisema Dkt.Turuka.
Aliongeza kwa kusema kuwa serikali imeidhinisha mpango wa maboresho wa mazingira wezeshi ya biashara na uwekezaji unaoainisha maeneo kumi yanayolenga taratibu za kisera,kisheria na za kiutawala zinazozingatiwa na wafanyabiahsra na wawekezaji.
Akisisitiza zaidi, Dkt. Turuka alisema, kuanzia mwaka 2003 hadi sasa serikali imefanya maboresho mbalimbali yakiwemo ya taasisi zake kufanya kazi kwa ubunifu na ushirikiano ili kuleta tija na ufanisi zaidi.
Akitolea mfano Bandari ya Dar es Salaam alisema huduma zote za ukaguzi wa ubora wa bidhaa kutoka nje ya nchi zinafanyika bandarini na zinahusisha mamlaka zote muhimu.
“Kwa mfano shughuli za Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na mamlaka nyingine zinafanyikia bandarini hapo ikiwa ni moja ya mikakati ambayo serikali imechukua katika kuboresha mazingira ya kufanya biashara”, Dkt. Turuka alisema.
Pia alisema muda wa kusajiri kampuni na kupata vibali mbalimbali hutolewa kwa muda mfupi sana ikilinganishwa na siku za hapo nyuma.
“Vituo vya ukaguzi wa mizigo barabarani vimepunguzwa kutoka hamsini hadi 15 ili kurahisisha usafirishaji wa bidhaa zinazoenda nje ya nchi,” alisema Dkt.Turuka na kuongeza kuwa serikali itaendelea kuchukua hatua mbalimbali zenye lengo la kuboresha zaidi mazingira ya kufanya biashara.
Mifumo ya ulipaji kodi inafanyika kwa njia rahisi za kieletroniki katika malipo ya kodi mbalimbali kwa kutumia simu za mkononi ili kupunguza gharama na usumbufu kwa wafanyabiashara kupata huduma zote za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Pamoja na Tanzania kufanya maboresho hayo, mashirika kimataifa ikiwemo Shirika la Kimataifa la Maendeleo ya Biashara (UNCTAD), Kongamano la Uchumi Duniani (WEF) na Benki ya Dunia (WB) yanasema Tanzania inahitaji kuboresha zaidi mazingira ya biashara na uwekezaji.
“Sisi kama Serikali tutaendelea kutumia tathimini zilizotolewa na mashirika hayo kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji hapa nchini na kufikia matarajio ya wafanyabiashara na wawekezaji,” alisema Bw. Turuka.
Alisisitiza kuwa maboresho hayo yanalenga kufikia dira ya taifa ifikapo mwaka 2025 nchi kuwa ya kipato cha kati.
Mwisho.

No comments: