Sunday, September 15, 2013

TPSF yawapa changamoto Vijana kuwa wabunifu,kutumia fursa ili kujiendeleza kuichumi



Na Mwandishi Wetu
Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF) imewataka vijana nchini kuwa wabunifu na kutumia fursa za kibiashara ili kukuza vipato vyao na pato la taifa.
Mwenyekiti wa taasisi hiyo, Bw. Reginald Mengi alisema hayo wakati wa hafla ya kumkabidhi  tuzo ya heshima Mwenyekiti na Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Helvetic Solar Contractors LTD, Mhandisi, Patrick Ngowi jijini, Dar es Salaam mwishoni mwa juma kama njia ya kutambua mafanikio aliyoyapata katika biashara.
“Vijana wanawajibu wa kutumia vipaji vyao na elimu kujiendeleza kibiashara ili waweze kukua kibiashara na kulisaidia taifa kuboresha ustawi wa jamii,”alisema.
Alisema kijana aliyetunukiwa tuzo hiyo ameweza kufanikiwa kibiashara akiwa na umri wa miaka 28, hivyo vijana wengine wanatakiwa kuiga mfano huo.
Alisema taifa linategemea vijana hivyo wanatakiwa kujituma ili waweze kuwa wafanyabiashara wakubwa na matajiri wasaidie jamii inayowazunguka.
Mkurugenzi Mtendaji wa TPSF, Godfrey Simbeye alisema kijana huyo amefanikiwa kupitia biashara ya ukandarasi wa kutumia teknolojia ya nishati ya jua (Solar Power contractor) kusambaza umeme.
“Kijana huyu kwa sasa anamiliki makampuni mbalimbali ya kusambaza na kutumia nishati ya jua katika nchi tatu za Afrika Mashariki,”
Alisema makampuni hayo yamejumuishwa kundi la makampuni ya Helvetic Group of Companies lenye jumla ya mapato ya mamilioni ya dola.
“Mwaka 2011 kampuni hizi zilikuwa na pato la sh. Bilioni 12 na mwaka huu inatarajia kufikia pato la bilioni 20,”
Aliongeza kusema kwamba TPSF imempatia tuzo hiyo kwa kutambua juhudi zake kibiashara na kupata tuzo mbalimbali za kimataifa kama mjasirimali mdogo.
Pia kupitia tuzo za kimataita alizopata, ameweza kuitangza nchi nje ya nchi kwamba watanzania wanaweza.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Bi. Regina Kikuli ambaye alimkabidhi tuzo kijana huyo alisema tuzo hiyo iwe ni chachu kwa kijana huyo kuzidi kupata mafanikio zaidi.
“Serikali inaendelea kujenga mazingira mazuri kwa wajasirimali na wawkezaji ili nchi izidi kukua kiuchumi,”
Mwenyekiti na Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Helvetic Solar Contractors LTD, Mhandisi Patrick Ngowi vijana wasikate tamaa wajitume na kutumia fursa zilizopo.
“Mimi nilianza nikiwa sina kitu niliona fursa nikakopa fedha kisha nikaanza kufanya biashara na leo nimefikia hapa,” alisema.
Tuzo hiyo iliandaliwa na TPSF kwa kutambua mafanikio ambayo kijana huyo ameyafikia kibiashara.
Mwisho.

No comments: