Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya
Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Bw. Godfrey Simbeye (kushoto) na Rais wa Umoja
wa Wafanyabiashara wa China Tanzania (CBCT), Bw. Zuang Zaisheng wakitiliana
saini mkataba wa ushirikiano kati ya pande hizo mbili katika hafla iliyofanyika
jijini Dar es Salaam leo (Jumatatu).
Wanaoshuhudia ni Mwenyekiti wa TPSF, Dkt. Reginald Mengi (waliosimama kushoto)
na Balozi wa China Tanzania, Balozi Lu Youqing.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya
Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Bw. Godfrey Simbeye (kushoto) akibadilishana
nyaraka ya makubaliano ya mkataba wa ushirikiano na Rais wa Umoja wa
Wafanyabiashara wa China Tanzania (CBCT), Bw. Zuang Zaisheng baada ya kutiliana
saini katika hafla iliyofanyika jijini Dar es Salaam leo (Jumatatu). Wanaoshuhudia ni Mwenyekiti wa TPSF, Dkt.
Reginald Mengi (wa pili kushoto) na Balozi wa China Tanzania, Balozi Lu Youqing
(wa pili kulia).
Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Taasisi ya sekta Binafsi nchini
(TPSF) imewashauri wafanyabiashara wa China kuingia ubia na watanzania kwa
faida ya nchi zote mbili.
Mwenyekiti wa TPSF, Dkt. Reginald
Mengi ametoa rai hiyo katika hafla ya kutiliana saini ya makubaliano ya kushirikiana
kati ya TPSF na umoja wa Wafanyabiashara wa China nchini Tanzania (CBCT).
“Tunapenda kuona wakishirikiana na wafanyabiashara
wa Tanzania hasa katika uwekezaji wa viwanda kwa lengo la kusaidia maendeleo ya
nchi hii,” alisema Dkt. Mengi mbele ya waandishi wa habari jijini Dar es Salaam
leo (Jumatatu).
Alisema kama wawekezaji wa China watakuja
na kuwekeza bila kuwashirikisha watanzania, uwekezaji huo utakuwa wa upande
mmoja na watanzania wataendelea kuwa masikini.
Alitoa changamoto kwa wawekezaji wa
China kuwekeza kwenye viwanda vya kuyaongezea thamani mazao ya Tanzania ili bidhaa
zake zipelekwe kwenye masoko ya China na nchi mbalimbali na kuuzwa kwa bei
nzuri.
“Pia wafanyabiashara wa China wafuate
sheria za nchi wanapoingiza bidhaa zao na kuzingatia ubora,” alisema.
Alisema makubaliano yaliyofikiwa kati
ya CBCT na TPSF yatazidi kuchochea mahusiano mema ya kijami, kisiasa na
kibiashara kati ya nchi hizo mbili.
Naye Balozi wa China nchini, Bw.Lu
Youqing alisema China na Tanzania zina historia ndefu za urafiki.
“Tuna ushirikiano mkubwa na sasa
mahusiano ya kibiashara yamekuwa makubwa sana,” alisema na kuongeza kuwa kwa
sasa kuna wafanyabiashara zaidi ya 500 wa Kichina hapa Tanzania.
Aliongeza kusema kuwa wameingiza
utalaamu na teknolojia katika uzalishaji katika kuelekea kwenye mapinduzi ya
viwanda.
Alisema mahusiano ya kibiashara kati
ya TPSF na CBCT ni chachu na ni moja ya hatua katika kukuza uchumi wa Tanzania.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji
wa TPSF, Bw.Godfrey Simbeye alisema wafanyabiashara wa China kupitia CBCT wamesaini
makubaliano hayo katika jitihada za kuimarisha ushirikiano na biashara hapa
nchini.
“TPSF ni chombo cha juu cha sekta
binafsi, wakiwemo wafanyabiashara wa ndani na wageni na ndicho kinacho wasemea
wote serikalini,” alisema.
Alisema makubaliano hayo
yatawawezesha wafanyabiashara hao kuweza kutoa maoni yao juu ya maswala
mbalimbali yanayowahusu kibiashara hapa nchini kupitia TPSF.
Aliongeza kusema taasisi yao
inaendelea kuzungumza nao ili CBCT iweze kuwa mwanachama kamili wa TPSF.
Rais wa CBCT, Bw. Zuang Zaisheng
alisema mahusiano hayo ya kibiashara yanalenga wafanyabiashara wa china na
Tanzania kuwa kitu kimoja kibiashara.
“CBCT itaendelea kuwaeleza
wafanyabiashara wake waje kufanya biashara Tanzania na kuwekeza zaidi huku wakiheshimu
utamaduni na sheria zilizopo,”alisema.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment