Mkurugenzi wa Idara ya Elimu ya Juu katika Wizara ya Elimu na
Mafunzo ya Vitendo, Prof. Sylivia Temu (katikati) akipokea zawadi kutoka kwa
Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Utawalana Fedha, Prof. Faustin Kamuzora
(kulia) wakati wa kongamano la tano la elimu ya juu jijini Arusha mwishoni mwa
wiki. Kushoto ni Kaimu Mwenyekiti wa
jopo la makamu wakuu wa vyuo vikuu na wakuu wa vyuo Tanzania (CVCPT) ambao ndio
walitayarisha kongamano hilo.
Naibu Makamu
Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Utawalana Fedha, Prof. Faustin Kamuzora (kulia)
akiongea jambo na Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU),
Prof. Magishi Mgasa wakati wa kongamano la tano la elimu ya juu jijini Arusha
mwishoni mwa wiki. Kongamano hilo
lilitayarishwa na jopo la makamu wakuu wa vyuo vikuu na wakuu wa vyuo Tanzania
(CVCPT).
Na Mwandishi wetu, Arusha
Wasomi nchini wamesisitiza umuhimu wa
taasisi za elimu ya juu katika kufanikisha utekelezaji wa mkakati kabambe wa
serikali wa Matokeo Makubwa Sasa.
Mkakati huo uliozinduliwa na Rais Jakaya
Kikwete mwezi Februari mwaka huu unalenga kufikia malengo katika vipaumbele vya
maendeleo ya nchi kwa muda maalum ambapo viongozi watatakiwa kuonyesha
walichofanikisha.
Akizungumza wakati wa kongamano la
tano la elimu ya juu jijini Arusha mwishoni mwa wiki, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu
Mzumbe, Utawala na Taaluma, Prof. Faustin Kamuzora alisema kuwa vyuo vikuu
vinafanya kazi na serikali na sekta za wazalishaji ambao ni watekelezaji
wakubwa wa mkakati huo.
Alisema Mkakati huo wa Matokeo
Makubwa Sasa ni muhimu sana kwa kuwa baadhi ya ajira zitakazozalishwa kutokana
na utekelezwaji wake zitachukuliwa na wahitimu wa vyuo vikuu.
“Ni kwa faida ya vyuo vikuu
kuhakikisha mpango huu unafanikiwa kwa faida ya nchi na pia kuwapatia ajira
nzuri wahitimu wake,” alisema.
Mada kuu ya mkutano wa mwaka huu
uliotayarishwa na jopo la makamu wakuu wa vyuo vikuu na wakuu wa vyuo Tanzania
(CVCPT) ni jinsi gani vyuo vikuu vinaweza kushirikiana na waajiri ikiwemo
viwanda na makampuni ili kujenga elimu ya juu endelevu Tanzania.
Vipaumbele vya mkakati huo wa
serikali ni pamoja na elimu, nishati, kilimo, usafiri, maji na maendeleo ya
raslimali watu.
Katika sekta ya elimu, mkakati huu
unalenga kuongeza ufanisi katika ngazi za chini za elimu za chekechea, shule za
msingi na sekondari.
Katika sekta hii, mkakati huo
unalenga kuongeza kiwango cha ufaulu kwa shule za msingi na sekondari hadi
kufikia asilimia 60 mwaka 2013, asilimia 70 mwaka 2014 na asilimia 80 mwaka
2015.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara
ya Elimu ya Juu katika Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Vitendo, Prof. Sylivia
Temu alisema kuwa taasisi za elimu ya juu zina wajibu kuhakikisha kuwa mkakati
huo unafanikiwa.
“Ni muhimu kwa
vyuo vikuu kuhakikisha mkakati wa Matokeo Makubwa Sasa unafanikiwa kwa
kuzalisha walimu wenye uwezo,” Prof. Temu aliyekuwa anaongea kwa niaba ya
Katibu Mkuu wa wizara hiyo alisema.
Alisema pia
vyuo hivyo vijiweke tayari kupokea wanafunzi toka shule za sekondari
watakaoongezeka kutokana na mkakati huo.
Alitoa mfano
kuwa wakati serikali inahitaji walimu 25,000 wa sayansi, inazalisha walimu
2,000 pekee kwa mwaka.
“Hiyo ni
changamoto kwa taasisi za elimu ya juu…ni lazima itafutiwe ufumbuzi kama kwali
tunataka kufanikiwa katika utekelezaji wa mkakati huu,” alisema.
Lengo kubwa la CVCPT ni kukutanisha
wadau wa elimu ya juu kwa upande mmoja na wadau wengine wa maendeleo nchini kwa
lengo la kujadiliana jinsi ya kuimarisha elimu ya juu na raslimali watu hapa
nchini.
CVCPT ilianzishwa mwaka 2005.
Wajumbe wa CVCPT ni makamu wakuu wa
vyuo vikuu pamoja na wakuu wa taasisi za elimu binafsi na vya umma pamoja na
katibu mtendaji wa TCU.
Kama mwenyekiti wa sasa wa CVCPT,
Chuo kikuu Mzumbe kimekua kikitayarisha kongamano hilo kwa mwaka wa pili
mfululizo sasa.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment