Na Mwandishi
wetu, Dar es Salaam
Tanzania
imeendelea kufanya vizuri katika kuvutia mitaji na kuongoza katika nchi za
Afrika ya Mashariki kwa mujibu wa ripoti ya hivi karibuni.
Ripoti ya uwekezaji
ya Rand Merchant Bank (RMB), 2013 inayotoa mwongozo wa mahali pa kuwekeza kwa
makampuni, inaonyesha kuwa kwa mara ya kwanza Tanzania imeishinda Kenya katika
kuvutia mitaji ya uwekezaji ya makampuni.
Akiongelea
ripoti hiyo mbele ya waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi
Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji nchini (TIC), Bi. Juliet Kairuki alisema kuwa
Tanzania imeshikilia nafasi yake katika kundi la nchi kumi bora zinazovutia
uwekezaji wa mitaji ya makampuni makubwa.
Kufanya
vizuri kwa Tanzania kunatokana na kuboreshwa kwa mazingira ya uwekezaji ikiwemo
jitihada mbalimbali zinazofanywa na serikali ya awamu ya nne chini ya Rais
Jakaya Kikwete.
“Ripoti hii
ni uthibitisho tosha wa jitihada zinazofanywa na serikali katika kuimarisha
mazingira ya uwekezaji na kuvutia mitaji kutoka nje na ndani ya nchi,” alisema
Bi. Kairuki.
Tanzania,
Kenya na Ethiopia ni nchi pekee zilizo katika kundi la nchi kumi zinazofanya
vizuri katika eneo hili la Afrika.
Kwa mujibu wa
ripoti hiyo, Tanzania imepanda nafasi moja na kuwa ya tisa wakati Kenya
imeshuka nafasi na kuwa ya kumi.
Pamoja na
kwamba Rwanda haiku katika nchi kumi bora, bado imeendelea kuwa kivutio na
kushika nafasi ya 14.
Nchi ya
Uganda ni ya 15, Mauritius 16, Angola 20, na Burundi imeshika nafasi ya 41.
Nchi ya
Afrika ya Kusini ndio inayoongoza kwa kuvutia uwekezaji ikifuatiwa na Nigeria
katika nafasi ya pili.
RMB inatumia
vigezo vikuu vitatu kuangalia swala zima la kuvutia uwekezaji katika kila nchi
kama ifuatavyo: ukubwa wa soko; ukuaji wa uchumi kwa maika mitano ijayo na
mazingira ya kazi katika nchi husika.
Kwa mujibu wa
ripoti hiyo, nchi za Afrika bado zina kazi kubwa ya kufanya kuvutia uwekezaji
duniani kulinganisha na nchi nyingine.
Bi. Kairuki
alisema ripoti hiyo inataka ushirikishwaji zaidi wa sekta binafsi ili kuvutia
zaidi mitaji toka kampuni na benki kubwa.
“Kwa mara
nyingine tena tunahamasisha ushiriki zaidi wa sekta binafsi katika ujenzi wa
nchi yetu,” alisema.
Alisema kuwa
pamoja na changamoto kubwa iliyopo kuifanya Tanzania kufanya vizuri zaidi,
TIC imefurahia ripoti hiyo na kusema
kuwa inaonyesha juhudi za serikali katika kujenga mazingira bora ya uwekezaji
na biashara.
Mwisho
No comments:
Post a Comment