Waziri Mkuu Mizengo Pinda (kushoto)
akiongea na Gavana wa kisiwa cha Anjouan, Comoro, Anissi Chamsidine (kulia) wakati wa kongamano la
uwekezaji kanda ya kaskazini jana mjini Tanga.
Wengine katika picha ni Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Bi. Chiku Gallawa (wa
pili kulia aliyesimama), afisa wa Anjouan, Bw. Allaoui Toihirdine
(katikati aliyekaa) na Naibu waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa, Bw. Aggrey Mwanri (wa pili kushoto).
Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha
Uwekezaji Tanzania (TIC), Bi. Juliet Kairuki (kulia) akiteta jambo na Naibu
Waziri wa Fedha, Bi. Saada Mkuya Salum wakati wa kongamano la uwekezaji kanda
ya kaskazini jana mjini Tanga. Kongamano
hilo la siku mbili limetayarishwa na TIC.
Na Mwandishi wetu, Tanga
Serikali imesema kuwa inatambua mchango wa sekta binafsi
katika kufikia maendeleo na kwamba itaendelea kuweka mazingira yanayofaa
kuiwezesha kutumia fursa za uwekezaji hapa nchini.
Waziri Mkuu Mizengo Pinda alisema hayo alipokua akifungua
kongamano la uwekezaji kanda ya kaskazini lililoanza jana mjini Tanga.
Waziri Mkuu alisema mchango wa sekta binafsi na wawekezaji
hasa wale wa ndani ni mkubwa sana na serikali inaendelea kujenga mazingira bora
ili uwekezaji uwe rahisi zaidi kwa faida ya pande zote mbili.
“Nitakuwa mtu wa mwisho kudhihaki mchango wa sekta binafsi
hasa ya ndani katika maendeleo ya nchi hii,” alisema.
Alisema sekta hiyo na wawekezaji watumie fursa ya mazingira
bora yanayojengwa na serikali kuhakikisha wanafanya kazi na kuendelea huku
akiitaja sera ya ushirikiano kati ya sekta binafsi na umma (PPP) kama moja ya
firsa hizo.
Alisifu Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kwa juhudi
ilizochukua kuratibu kongamano hilo la kanda ya kaskazini na kutangaza fursa
zake ambazo amesema bado hazijatumiwa vya kutosha.
Alieleza kuwa kongamano kama hizo ni muhimu sana katika
kuwasiliana na wawekezaji na kuangalia jinsi wanavyoweza kushirikiana na
serikali kuleta maendeleo.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu,
Uwekezaji na Uwezeshaji, Dkt. Mary nagu alisema uwekezaji ni njia moja wapo
muhimu katika kugeuza fursa kuwa na kuwa maendeleo.
Alitoa wito kwa viongozi wa mikoa katika kanda hiyo ya
kaskazini kuhakikisha kuwa wanashughulikia pia maendeleo ya uchumi na uwekezaji
katika maeneo yao ili kuleta mapinduzi ya uchumi haraka.
“Hii itasaidia kufikia maendeleo kwa haraka zaidi,” alisema.
Akiwasilisha mada kuhusu fursa zinazopatikana katika kanda ya
kaskazini, mhadhiri mwandamizi toka Taasisi ya Maendeleo, Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam, Prof. Suleiman Ngware alisema wawekezaji wawe na uhakika wa faida
wanapokuja Tanzania kwa sababu ya amani na utengamano wa kitaifa uliopo.
“Pamoja na amani, kanda hii na nchi nzima ina raslimali za
kutosha na fursa mbalimbali kwa wawekezaji,” alisema.
Mkuu wa mkoa wa Tanga, Bi. Chiku Gallawa alikaribisha
wawekezaji katika mkoa wake na kanda ya kaskazini na kuwahimiza kutumia fursa.
“Tunawahakikishia ushirikiano mkubwa,” alisema.
Kongamano hilo la siku mbili lilivutia wawekezaji zaidi ya
1,500 linahudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali, sekta binafsi, viongozi
wa dini, mabalozi na wadau wengine wa maendeleo.
Pia, Gavana wa kisiwa cha Anjouan, moja ya visiwa vinavyounda
nchi ya Comoro, Anissi Chamsidine anahudhuria kongamano hilo.
Mikoa inayounda kanda ya kaskazini ni pamoja na Tanga,
Manyara na Arusha.
Baadhi ya vivutio katika kanda ya kaskazini ni ardhi yenye
rutuba kwa kilimo cha mazao ya biashara, mbogamboga na matunda, madini, na
utalii.
Mwisho
No comments:
Post a Comment