Na Mwandishi wetu, Tanga
Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kimesisitiza kuwa
kitaendelea kutoa ushirikiano kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi wanaotaka
kuwekeza katika mikoa ya kanda ya kaskazini na maeneo mengine nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa kongamano la
uwekezaji kanda ya kaskazini lililomalizika hivi karibuni mjini Tanga,
Mkurugenzi Mtendaji wa kituo hicho, Bi. Juliet Kairuki alisema kuwa kituo chake
kiko tayari kupokea wale wote walio tayari kuwekeza katika kanda hiyo.
“Kwa wale ambao watakuwa tayari kuwekeza katika mikoa ya
kanda ya kaskazini, milango ipo wazi kuandikisha miradi yao TIC,” alisema mjini
Tanga hivi karibuni.
Akielezea kongamano hilo ambalo ni la kwanza kufanyika katika
kanda hiyo alisema huo ni mwanzo wa juhudi kama hizo katika kutangaza vivutio
vya uwekezaji katika kanda hiyo na maeneo mengine ya nchi.
Alitoa shukrani kwa mikoa ya kanda hiyo kwa kushirikiana
katika kongamano hilo na kusema kuwa hiyo ni njia nzuri na yenye matokeo
makubwa na mazuri kwa uchumi wao na wa nchi kwa ujumla.
Alisema kongamano hilo limetoa fursa nzuri kwa wawekezaji,
wafanyabiashara na wajasiriamali kufahamu fursa mbalimbali za uwekezaji zilizo
katika mikoa ya kanda ya kaskazini na pia kuelezea ambavyo serikali inasaidia
uanzishwaji wa miradi ya uwekezaji.
Alisema katika kipindi cha miaka 12 iliyopita, Tanzania
imefanya vizuri katika eneo la uwekezaji ambapo uwekezaji mkubwa umefanywa
kwenye sekta za kilimo, utalii, viwanda, mawasiliano, miundombinu na
usafirishaji.
Alisema katika kipindi hicho, miradi ya uwekezaji imekuwa
kutoka 178 hadi 869 mwaka 2012 huku uwekezaji uliofanywa na watanzania wenyewe
ukiwa ni asilimia 53 ya miradi yote.
Alifafanua kuwa kuongezeka kwa miradi kumechangia kukua kwa
mitaji kutoka dola za kimarekani 874 milioni hadi USD 12 bilioni.
“Miradi hii imevutia ajira mpya zinazofikia 135,760 mwaka
2012,” alisema.
Mkuu wa wilaya ya Hanan’g, mkoa wa Manyara, Bi. Christina
Mndeme alisema kongamano hilo limekuwa la manufaa makubwa kwa wilaya yake.
Alisema kutokana na kongamano hilo, tayari amefikia
makubaliano na baadhi ya wawekezaji ambao wako tayari katika kujenga kiwanda
cha kuongeza thamani mazao mbalimbali pamoja na mwekezaji mwingine, Manyara
Cement, anayetaka kujenga kiwanda cha sementi.
“Makongamano kama haya ni muhimu sana, tuko tayari kufanya
kazi na wawekezaji na TIC,” alisema.
Awali, akielezea umuhimu wa makongamano hayo ya uwekezaji,
Waziri Mkuu Mizengo Pinda alisema ni ya muhimu na kuwa yanatakiwa kuimarishwa
zaidi.
Akitoa mfano alisema tayari matokeo mazuri yameshaonekana
kutokana na kongamano la uwekezaji lililofanyika mwezi Oktoba mwaka 2012 katika
kanda ya Nyanda ya Juu Kusini mkoani katavi.
“Sasa kuna ongezeko kubwa la vyumba vya hoteli vinavyofikia
elfu moja kutokana na uwekezaji katika sekta ya utalii katika mkoa wa Katavi,”
alisema.
Kongamano la uwekezaji kanda ya kaskazini lilihudhuriwa na
wawekezaji zaidi ya 1,500 toka ndani na nje ya nchi pamoja na maafisa wengine
toka sekta binafsi na umma, viongozi wa dini, mabalozi na wadau wengine wa maendeleo.
Mwisho