Tuesday, March 25, 2014

Watanzania washauriwa kujenga utamaduni wa kusoma, kuandika vitabu

Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Watanzania wameshauriwa kujenga utamaduni wa kusoma vitabu ili kuchota maarifa mbalimbali na kuwasaidia katika kufanya shughuli mbalimbali za maendeleo.

Wito huo ulitolewa na mwandishi wa vitabu, Bw. Evodius Katare ambaye pia ni Kaimu Mkurugenzi wa Utawa na Fedha wa Wakala wa Mradi wa Mabasi yaendayo haraka (DART) akiongea na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam.

“Watanzania wakijenga utamaduni huu wa kusoma vitabu itawasaidia sana kimaisha,” alisema na kuongeza kuwa kusoma vitabu ni kuchota maarifa mbalimbali kutoka kwa waandishi.

Akitoa mfano alisema watu wakipenda kusoma vitabu pia watapenda kuandika vitabu ili wengine waweze kusoma.
Alisema yeye anapenda kusoma vitabu na utamaduni huo umemsaidia pia kuwa na tabia ya kuandika vitabu.

“Tabia ya kusoma vitabu imenisaidia kuwa mwandishi wa vitabu japo taaluma yangu siyo mwandishi,” alisema.

Kitabu chake kipya kinaitwa “Julius Nyerere, Falsafa zake na dhana ya Utakatifu.”

Alisema ameandika kitabu hicho kutokana na Kanisa Katoliki kutangaza mchakato wa kumfanya Baba wa taifa, Mwalimu Nyerere kuwa mtakatifu na uelewa mdogo wa jamii hasa vijana kuhusu mchango wake kwa taifa hili.
Anaungana na kanisa hilo kwa kutaka kumpatia zawadi hiyo kubwa Nyerere na kwamba anastahili kuipata kutokana na matendo yake ya uongozi aliyoifanyia nchi hii.

“Mwalimu Nyerere alikuwa mwanasiasa na kiongozi aliyeifanya jamii ya watanzania kuwa sehemu ya familia yake na hiyo ikawa tunu kwenu ya uwepo wa amani na utulivu,”alisema Bw.Katare.

Alisema katika kipindi chote cha uhai wake alitumia muda wake kuwatumikia watanzania, aliongoza harakati za kuikomboa nchi na pia aliliongoza taifa kwa uadilifu baada ya uhuru.

Alisema kitabu hicho kitaiwezesha jamii hasa vijana ambao hawakuishi kipindi cha Mwalimu kumfahamu ili wawe na fursa nzuri wanapotaka kumfananisha na wanasiasa wanaojitokeza leo ambao wengi wanajali familia na maslahi yao tu.

Alieleza kuwa watu wasome kitabu chake hicho ili  waweze kumfahamu zaidi mwalimu Nyerere na mchango wake kwa taifa hili.

“Kitabu hiki kitasaidia pia vizazi vijavyo kufahamu historia nzuri juu ya Mwalimu Nyerere,”alisema Bw.Katare

Alisisistiza kwamba tabia ya kusoma na kuandika vitabu hujengwa tangu awali vijana wakiwa wadogo katika mashule.

Alisema kuna kila sababu ya Tanzania kujenga maktaba shule zote za msingi na sekondari na kuwa na walimu wa kuhamasisha wanafunzi kusoma vitabu ili kuwa na jamii bora zaidi.


Mwisho.

No comments: