Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mradi wa Mabasi yaendayo
Haraka (DART Agency), Bi. Asteria Mlambo akisisitiza jambo kwa waandishi
wa habari jana jijini Dar es Salaam alipokuwa akiongelea utaratibu utakaotumika
kupata watoa huduma wa mradi huo utakapoanza.
Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Wakala wa Mradi wa Mabasi yaendayo aaraka (DART)
umesema kabla ya utekelezaji wa awamu ya kwanza ya mradi kukamilika, mwaka huu
kutakuwa na mabasi machache ambayo yataanza kutoa huduma ya usafiri kutoka
Kimara hadi Kivukoni.
Kaimu Mtendaji Mkuu wa (DART), Bi. Asteria Mlambo aliwambia
waandishi wa habari jijini Dar es Salaam hivi karibu kuwa utekelezaji wa awamu
ya kwanza unaendelea vizuri na kabla ya kukamirika hapo mwakani,kutakuwa na mabasi
machache yataanza kufanya kazi mwaka huu.
“Mradi huu wa mabasi haya unatarajia kukamilika mwaka
ujao lakini juhudi zinafanyika kuhakikisha mwaka huu yanapatikana mabasi
machache kuanza kutoa huduma,”alisema Bi. Mlambo.
Alisema utekelezaji wa mradi huu umegawanyika katika awamu
sita katika jij la Dar-es-salaam ambapo kwa sasa wapo katika awamu ya kwanza na
inaendelea vizuri.
“Katika awamu hii ya kwanza wakandarasi wapo katika
mafungu makuu sita, ambapo fungu la kwanza ni ujenzi wa barabara unaofanywa na
kampuni ya strabag ya ujerumani kuanzia Kimara hadi Kivukoni,” alisema.
Fungu la pili ni kituo kikuu cha mabasi cha Ubungo
ambako kunaajengwa maegesho na karakana
ya mabasi kwa ajili ya kufanyia mabasi matengnezo.
Bi. Mlambo alisema fungu la tatu ni ujenzi wa kituo
cha maegesho eneo la jangwani ambacho pia kutajengwa makao makuu ya mradi kwa
ajili ya maswala ya kiutawala.
Alisema fungu la nne ni eneo la kivukoni ambako ujenzi
wake umefikia asilimia 90, fungu la tano ni ujenzi kituo kikuu eneo la Kariakoo
Gerezani Quarter na fungu la sita ni vituo vidogo ambavyo vitashusha na kupakia
abiria
“Vituo hivi vidogo vitawaunganisha abiria kutoka
maeneo wanayoishi na mfumo wa mabasi haya,”alisema mtendaji mkuu huyo na kuongeza kuwa maendeleo
ya ujenzi wa mradi yanaridhisha.
Akifafanua zaidi alisema mpaka hivi sasa utekelezaji
wa mradi huo upo katika kiwango cha 55% ya ujenzi wa miundombinu unasimamiwa na
Wakala wa Usimamiaji wa Barabara nchini (TANROADS).
“Kampuni ya ushauri ya Rebel Group kutoka Uholanzi ambayo
ilishanda zabuni itasaidia kupata watoa huduma baada ya kutangazwa tenda hiyo
hapo mwezi mei, mwaka huu,” alisema.
Alisema katika utekelezaji mradi huo wakala ulikutana
na changamoto mbalimbali ikiwemo ya kuwepo kwa huduma mbalimbali zilizokuwa
zinaendeshwa kando ya barabara ambapo wakala ulilazimika kuingia gharama
kuviondosha.
Wakala wa Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka ambao upo
chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu Serikali za Mitaa na Tawala za mikoa (TAMISEMI) unatekeleza
maradi wa mabasi hayo ili kutatua kero ya msongamano wa magari katika jiji la
Dar es Salaam.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment