Monday, March 31, 2014

Wamiliki wa daladala watakiwa kujiandikisha DART

Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam

Wakala wa Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka Dar es Salaam (DART) umewataka wamiliki wote wa mabasi ya abiria maarufu kama daladala ambao mabasi yao yanapita katika barabara ya Morogoro au kukatiza katika njia hiyo kufika katika ofisi zake kujiandikisha.

Mhandisi wa Wakala huo, Bw. John Shauri aliwaambia waandishi wa habari  jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki kuwa wamiliki hao wa daladala wanatakiwa kufika katika ofisi za DART zilizopo jengo la Ubungo Plaza barabara ya Morogoro eneo la Ubungo kuanzia tarehe 31 mwezi huu hadi tarehe 21 mwezi April mwaka huu kwa ajili ya kujiandikisha kama moja ya matayarisho ya kupisha mradi huo.

Kwa sasa wakala huo uko kwenye mchakato wa kuwezesha upatikanaji wa watoa huduma kwenye mfumo mpya wa mabasi yaendayo haraka awamu ya kwanza ambayo inajumuisha barabara ya Morogoro, Kawawa na mtaa wa Msimbazi kwa njia kuu na nyingine za kiungo. 
Alisema kulingana na mpango wa uendeshaji wa mfumo wa DART, barabara zinazohusika zitapaswa kutumiwa na mabasi ya mfumo huo pekee.
“Wakala umemwajiri mtaalamu mshauri ili kuwawezesha wamiliki wa daladala kuuelewa vizuri mfumo na kujipanga kuwa washiriki kwenye mfumo huu mpya,” alisema.
Kwa mujibu wa Bw. Shauri, jumla ya njia 64 zitakoma kutumika kutokana na kuanza kwa mradi huo.

Alitaja baadhi ya njia zitakazoguswa na zoezi hilo kuwa ni pamoja na Mbagala Rangi 3 kwenda Masaki, Vingunguti kwenda Makumbusho, Kunduchi Kwenda Mwenge, na Msata kwenda Ubungo.

Njia nyingine ni Kariakoo kwenda Makumbusho, Buguruni kwenda Kawe, Kivukoni kwenda Mburahati, Mbagala kuu kwenda Mwenge, na Mkata kwenda Ubungo.

Njia nyingine ni Mburahati kwenda Muhimbili, Segerea kwenda Mwenge, Vingunguti kwenda Kawe, Vingunguti kwenda Mbezi, Kunduchi kwenda Posta, na Kunduchi kwenda Makumbusho.

Pia alizitaja Temeke kwenda Masaki, Kivukoni kwenda Mabibo, Muhimbili kwenda Mabibo, Posta kwenda Ubungo, Posta kwenda Mabibo, Kawe kwenda Kimara, Kivukoni kwenda Mbezi, Mwenge kwenda Mbezi, Posta kwenda Mbezi, Mbezi kwenda Tegeta na Bunju kwenda Makumbusho.

Alisema wamiliki hao wa daladala wanahitaji kwenda na nakala ya leseni ya SUMATRA, nakala ya usajili wa gari, na nakala za rangi za leseni za madereva wao.

Uandikishaji utakuwa unafanyika kuanzia Jumatatu hadi Ijumaa asubuhi saa tatu mpaka saa 11 jioni.  Kwa siku za Jumamosi na Jumapili uandikishaji utakuwa unafanyika kuanzia saa tatu asubuhi mpaka saa nane na nusu mchana.

Naye Mshauri Elekezi wa Wakala huo, Bw. Felix Mlaki alisisitiza wamiliki hao kufika ofisi za DART kujisajiri na kufafanua kuwa daladala hazitasajiliwa tena na SUMATRA katika eneo la mradi huo.

“Tunawahitaji wajisajili na pia watoe mawazo yao juu ya kuanza kwa awamu ya kwanza ya mradi huu wa mabasi yaendayo haraka,”alisema Bw. Mlaki.

Alisema mradi huu ni wa kisasa na una manufaa makubwa kwa wananchi.

Alisema mfumo huo unatoa utaratibu mzuri wa ukataji tiketi na utoaji taarifa sahihi kwa abiria.


Mwisho

No comments: