Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Wadau na watumiaji mbalimbali wa Bandari ya Dar es
Salaam wamepongeza maboresho yaliyofanywa na serikali katika bandari hiyo na
kuelezea kuridhishwa na ufanisi wa huduma zinanavyo tolewa kwa sasa.
Mbali ya kupongeza maboresho hayo, wadau wameridhishwa
na hatua mbalimbali ambazo serikali kupitia Menejimenti ya Mamlaka ya Usimamizi
wa Bandari nchini (TPA)kuanza kufanya kazi masaa 24.
“Hii ni dalili njema kwa uchumi wa nchi yetu na nchi jirani,”
Mkurugenzi wa kampuni inayojishughulisha na huduma za mizigo bandarini hapo,
Reindeer Investment Limited, Bw. Mlimuka Luhanga aliwaambia waandishi wa habari
jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.
Bw. Luhanga alisema juhudi za kuiimarisha bandari ya
Dar es Salaam zinaiweka Tanzania katika nafasi nzuri ya ushindani katika eneo
hili la Afrika na kusema kuwa kama kazi hiyo ikifanywa vyema itakuwa faida
kubwa kwa wafanyabiashara wa ndani na nje pamoja na nchi kwa ujumla.
Hata hivyo Bw. Luhanga ameipa changamoto serikali
kuimarisha zaidi usafiri wa reli nchini kwani utasaidia kwa kiasi kikubwa
kusafirisha bidhaa zinazopakuliwa bandarini na kuzisafirisha sehemu husika.
“Kwa kutumia barabara tu hatuwezi kufanikisha
kusafirisha mizigo yote kwa wakati na vilevle barabara zetu hazitadumu kwa muda
mrefu hivyo miundombinu ya reli itasaidia sana kusafirisha mizigo ndani na nje
ya nchi jirani,” alisema mkurugenzi huyo.
Naye Bw.Safari Kazimoto ambaye anajishughulisha na
shughuli ya uingizaji magari kutoka nje na kuyauza amesifu maboresho ya huduma
ya bandari na kusema yamerudisha imani kubwa kwa watumiaji wa bandari ya Dar es
Salaam.
“Kwa miezi ya karibuni biashara yangu imeimarika
kutokana na ufanisi katika bandari na vilevile imepunguza msongamano na kuleta
imani kwa watumiaji wa bandari ya Dar es Salaam,”alisisitiza Bw. Kazimoto.
Kwa upande wake Bw. Pierre Nzwagiba ambaye ni
mfanyabiashara kutoka Congo DRC, aliwaambia waandishi wa habari kuwa bandari ya
Dar es Salaam ni bandari kubwa na
inauwezo mkubwa wa kupitisha mizigo mingi na maboresho yaliyofanywa hivi
karibuni yataimarisha biashara.
“Naipongeza TPA kwa kuchukua hatua za makusudi kwa
makusudi kuhakikisha imani ya watumiaji wa bandari hii wanarudi na wanaendelea
kutumia huduma kama kawaida,” alisema Nzwagiba.
Raia huyo wa Congo DRC, ameitaka serikali kuendelea
kuwekeza zaidi katika miundombinu na uboreshaji wa huduma bandarini na kutoridhika
na maboresho hayo tu.
Katika miaka ya hivi karibuni pamekuwepo na mikakati
mbalimbali inayofanywa na serikali kupitia Wizara ya Uchukuzi, TPA pamoja na
wadau wengine kuhakikisha kuwa bandari ya Dar es Salaam inatoa huduma bora kwa
wateja wa hapa nchini pamoja na wale wan chi jirani.
Kutokana na mikakati hiyo pamekuwepo na ongezeko la
shehena, tija katika kuhudumia shehena na meli zinazotumia bandari hiyo, na
kupungua kwa msongamano wa meli.
Pia kumekuwepo na punguzo kubwa la mrundikano wa
mizigo na kufanikiwa kukomesha vitendo vya upotevu wa mizigo na wizi kwa kiasi
kikubwa.
Kwa mfano, kwa upande wa mapato, mwaka 2012/13 wastani
wa Tshs bilioni 371.7 zilikusanywa, sawa na ongezeko la asilimia 14.3
ukilinganisha na Tsh. bilioni 325.3 mwaka 2011/12.
Katika mapato hayo, bandari bila ya makusanyo ya
TICTS, ilikusanya Tsh.bilioni 324.5 mwaka 2012/13, ikiwa ni ongezeko la
asilimia 18.9, ikilinganishwa na mapato ya Tsh.bilioni 272.9 mwaka 2011/12.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment