Thursday, March 13, 2014

EPZA yatoa msaada Polisi Dar es Salaam

Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa  Mamlaka ya ukanda maalumu wa uwekezaji (EPZA), Bw. Desidery Kalimwenjuma (kushoto) akimkabidhi Mkuu wa  polisi wilaya ya kimara, SP Cosmas Papalika (katikati) moja ya vifaa vitakavyotumika kwa ajili ya ukarabati wa kituo kidogo cha polisi cha Mwongozo kilichopo Makuburi Kibangu jijini Dar es Salaam jana.  Wengine ni afisa wa polisi, Ali Rashidi (kulia), Mkuu wa kituo cha hicho, John Haule (wa pili kulia) na Mkuu wa kitengo cha manunuzi kutoka EPZA Bw. Joseph Matara (wa pili kushoto).
Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Mamlaka ya Ukanda Maalumu wa Uwekezaji (EPZA) imetoa msaada wa vifaa vya ujenzi vyenye thamani ya Tshs 1,500,000 kwa Kituo cha Polisi Mwongozo, Makuburi Kibangu kwa ajili ya kukifanyia ukarabati.

Akikabidhi msaada huo Mkurugenzi wa Utawala na Fedha wa Mamlaka hiyo, Bw. Desidery Kalimwenjuma alisema msaada huo unalenga kukiboresha kituo hicho ambacho kipo karibu na mamlaka yao.

“Tunatambua suala la usalama katika maeneo ya uzalishaji,” alisema jana jijini Dar es Salaam na kuongeza kuwa hali hiyo iliwasukuma kutoa msaada wa vifaa vya ujenzi ili waweze kukarabati jengo hilo la kituo.

Alisema misaada ambayo mamlaka imetoa kwa kituo hicho ni pamoja na milango, , rangi za maji na za mafuta.

“Eneo la mamlaka yetu ni eneo maalumu la uwekezaji na linahitaji usalama zaidi,”aliongeza kusema Bw. Kalimwenjuma.

Alisema msaada huo pia ni sehemu ya kujenga mahusiano mena kati ya mamlaka, jeshi la polisi kupitia kituo hicho na serikali ya mtaa ya Makuburi Kibangu.

Alisema mamlaka inaahidi kuzidi kutoa misaada ya vifaa kama ilivyofanya kwa ajili ya kuboresha jengo la kituo hicho ambalo linahitaji matengenezo.

Mkuu wa Polisi Wilaya ya Kipolisi ya Kimara, SP Cosmas Papalika aliipongeza mamlaka hiyo kwa kutoa msaada huo. “Kiujumla hali ya usalama katika eneo hili ni nzuri, hakuna matukio ya kihalifu kama ilivyo kuwa huko nyuma,” alisema na kufafanua kuwa hilo linatokana na na ushirikiano unaotolewa na jamii katika eneo hilo.

Alisema kituo hicho na vile vyote katika  wilaya yake vinahitaji ushiriki wa jamii katika kuhakikisha vinaboreshwa zaidi na kutoa huduma nzuri.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa ya  Makuburi Kibangu, Bw. Moshi Kaftanyi liishukuru  mamlaka hiyo kwa kuitikia wito wa kusaidia kituo hicho cha polisi ambacho kipo katika mtaa wake.

“Kituo hiki kilikuwa kimechakaa, na tukaamua kuiomba mamlaka  isaidie ili kuweza kufanya marekebisho,” alisema na kuongeza kuwa moyo huo unatakiwa kuigwa na taasisi mbalimbali na jamii pia.

Alisema usalama mahali pa kazi na makazi ni muhimu sana, hivyo kunakila sababu ya kuhakikisha jamii na taasisi zinasaidia vituo vya polisi.


Mwisho.

No comments: