Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Wafanyabiashara wenye vibanda vya kukatia
tiketi katika stendi ya Ubungo ambako Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) unaendelea,
wametakiwa kuviondosha vibanda hivyo katika maeneo hayo ili kupisha ujenzi wa
mradi huo.
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala
za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Bw. Jumanne Sagini aliwaambia
waandishi wa habari mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam kuwa wafanyabiashara
hao wanatakiwa kuondoa vibanda vyao ili kupisha ujenzi wa mradi huo unaoendelea
katika eneo hilo.
“Tunataka waondoe vibanda vyao katika
eneo la Ubungo ili kupisha mradi unaoendelea uweze kukamilika kwa muda tulioupanga,”
alisema Bw. Sagini.
Alisema wafanyabiashara hao
walishalipwa fidia baada ya kufanyiwa tathimi lakini cha kushangaza bado
wanaendelea kuwepo katika maeneo hayo na kusababisha mradi kutoendelea kwa kasi
iliyokuwa inakusudiwa katika eneo hilo.
Alisema serikali ililipa Jiji la Dar
es Salaam fedha kwa ajili ya kuwapatia fidia wao, na uongozi wa jiji ulifanya hivyo
na kila mtu alipata fidia hiyo.
“Kwa vile uongozi wa Jiji la Dar es Salaam uliwalipa
fidia wenye vibanda,sasa wanapaswa kusimamia zoezi hili na kuwaondosha kabisa
hao waliobaki kwa sababu hawastahili kuwepo tena katika maeneo haya,”aliongeza
kusema Bw. Sagini.
Alisema
dhamira ya serikali ni kuona mradi huo unakamilika kwa muda uliopangwa kwa sababu
ukichelewa kwa makosa ya hapa nchini, serikali itaingia gharama ya kumlipa
mkandarasi kwa kuchelewesha mradi.
Naye Kaimu
Mtendaji Mkuu wa Mamlaka inayosimamia mradi huo ya DART,Bi. Asteria Mlambo alisema
maeneo yote ya Ubungo wakati mradi unaanza kulikuwa na majengo mbalimbali
zikiwemo hoteli na vibanda vya kukatia tiketi.
“Maeneo
haya yote yameshafidiwa thamani ya Tsh milioni 260 kupisha mradi kuendelea kujengwa,” aliongeza kusema, Bi.
Mlambo.
Hivi karibuni DART iliingia mkataba na kampuni ya washauri
itakayofanya kazi ya kupatikana watoa huduma muhimu kwa mradi huo unaotarajiwa
kuanza mwishoni mwa mwaka huu.
Hatua hiyo ilifikiwa baada ya kampuni
hiyo ya REBEL Group ya Uholanzi kushinda zabuni na kushindanishwa na kampuni
nyingine.
Mradi huu unalenga kupunguza kwa
kiwango kikubwa foleni na msongamano wa magari katika jiji la Dar es Salaam.
Barabara zinazohusika na awamu hii ni
pamoja na kilomita 20.9 kutoka Kimara hadi Kivukoni; barabara ya Msimbazi
kutoka Faya hadi Kariakoo-Gerezani na sehemu ya barabara ya Kawawa kuanzia
Magomeni hadi Morocco.
Mwisho
No comments:
Post a Comment