Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Utawala na Fedha,
Prof. Faustin Kamuzora (kushoto) akipokea zawadi toka kwa Naibu Makamu Mkuu wa
Chuo Kikuu cha Bradford cha Uingereza jana jijini Dar es Salaam. Anayeshuhudia ni Prof. George Shumbusho wa
Mzumbe Timu ya watu wanne toka Bradford ilikuwa Mzumbe kutathmini maendeleo ya
ushirikiano wao wa muda mrefu.
Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Chuo Kikuu Mzumbe na kile cha Bradford cha Uingereza
vimedhamiria kuimarisha uhusiano zaidi kwa faida ya vyuo hivyo na nchi kwa
ujumla.
Hatua hii inakuja wakati ambapo timu ya watu wanne toka chuo
hicho maarufu cha Uingereza ikiwa Mzumbe kufanya tathmini ya kawaida ya kila
mwaka kuona jinsi ushirikiano wao unavyoendelea.
Katika ushirikiano huo, Mzumbe inafundisha kozi mbili ambazo
wanafunzi wanaohitimu hupatiwa vyeti vya chuo hicho cha Uingereza.
Kozi hizo ambazo zilianza kutolewa chini ya program ya
ushirikiano huo mwanzoni mwa mwaka 2011 ni Shahada ya uzamili katika uchumi na
fedha na shahada ya uzamili katika maendeleo ya sera na asasi za kiraia.
“Tunataraji kuwa tunaweza kuendelea kuimarisha ushirikiano
huu na wanafunzi hapa Mzumbe,” Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Bradford,
aliwaambia waandishi wa habari jana.
Alisema kwa pamoja, chuo chake na Mzumbe wanataka kuleta
mabadiliko bora kwa wanafunzi na kuwajengea fursa na hivyo kufikia maendeleo
endelevu na kufanya dunia kuwa mahali bora pa kuishi.
Akizungumzia kuhusu program hiyo, alisema wanafunzi wanafanya
vyema na kusaidia chuo chao kuendelea kushikilia nafasi bora katika kufundisha
kozi hizo.
Kwa upande wake, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe,
Utawala na Fedha, Prof. Faustin Kamuzora alifafanua kuwa tathmini hiyo
inayofanyika kila mwaka inalenga kuhakikisha kuwa ubora wa kozi zinazotolewa
zinaendelea kuwa nzuri na kuboresha zaidi pale inapotakiwa.
“Tunaendelea vyema na ushirikiano huu, tunatarajia kupanua
zaidi maeneo ya ushirikiano wetu,” alisema.
Alitaja maeneo ambayo wanatarajia kishirikiana zaidi kama
kuanzisha kozi mpya, kufanya tafiti kwa pamoja, kupeleka wanafunzi wa uzamivu
katika chuo hicho kwa masomo zaidi na kuwajengea zaidi uwezo walimu wa Mzumbe
kupitia mafunzo mbalimbali.
Mratibu wa program hiyo Mzumbe, Dk. Andrew Mushi alisifu
ushirikiano huo na kusema kuwa umesaidia kuinua hadhi ya Mzumbe pamoja na kutoa
wahitimu walio bora kabisa kimataifa.
“Wahitimu wanaomaliza kozi hii wanafanya vizuri sana katika
kazi zao,” alisema.
Ushirikiano kati ya vyuo hivi umedumu sasa kwa miaka
takribani 30 wakishirikiana katika maeneo mbalimbali.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment