Monday, March 17, 2014

Mkandarasi wa mradi wa barabara ya mabasi yaendayo haraka aruhusu maeneo yakugeuka

MSHAURI Mkuu wa Ufundi wa Wakala wa Mradi wa Mabasi yaendayo Haraka (DART), Bwana Dieter Schelling (kulia) akifafanua jambo kwa waandishi wa habari (ambao hawapo pichani) eneo la Kimara kuwa Kampuni ya STRABAG kuruhusu vituo tano vitumike kugeuzia magari (U-turns) mpaka vituo vya kudumu vitakapokamilika ndani ya miezi sita. Kushoto ni Mhandisi wa DART, Mhandisi John Shauri
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

KAMPUNI ya ujenzi wa barabara ya STRABAG  inayoendelea na ujenzi kwa ajili  ya mradi wa mabasi yaendayo haraka umeruhusu upande mmoja wa barabara uliokamilika kutumika ili kupunguza foleni  ya magari yanayoka Kimara kuelekea katikati ya jiji au sehemu nyingine kupitia  barabara ya Morogoro.  

Mhandisi wa Wakala wa Mradi wa Mabasi yaendayo Haraka (DART),Mhandisi John Shauri aliwaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki kwamba mbali ya kuruhusu upande mmoja wa barabara, kampuni ya STRABAG imeruhusu pia vituo vitano vitumike kwa kugeuzia magari kwa muda wa miezi sita (provisional U-turns) mpaka maeneo matatu ya kudumu yatakapo kamilika katika kipindi hicho.

“Kuruhusu upande mmoja kutumika na pia maeneo ya kugeukia magari kumesaidia sana kupunguza foleni kwa magari yanayotoka kimara kwenda Ubungo nay ale yanayotoka Ubungo kwenda Kimara,”alisema Mhandisi Shauri.
Mhandisi huyo amewataka madereva kuwa waangalifu na mwendo kwani wastani wa mwendo unaotakiwa ni spidi 50 tu na si vinginevyo kwani mwendo kasi utasababisha ajali zisizo za lazima.

“Mwendo wa kawaida utasaidia sana maeneo ambayo yameruhusiwa magari kugeuka na na kuelekea sehemu husika bila kusababisha ajali,” alisema na kuongeza kuwa mradi utakapokamilika utapunguza kabisa foleni na msongamano wa magari.

Mhandisi Shauri ambaye aliambana na Mshauri Mkuu wa Ufundi wa Mradi huo, Bwana Dieter Schelling, alivitaja vituo hivyo vitano vya kugeuzia kuwa ni Kimara Corner,Kimara Baruti, katikati ya Kimara Butcher na Kimara kwa Thomas, Kimara Resort na Kimara mwisho.
“Kwa sasa magari katika barabara hii ya Morogoro magari yanapita pasipo msongamano mkubwa kama ilivyokuwa awali na kurahisisha watu kutoka Mbezi,Kibamba kuwahi kwa wakati katika shughuli zao,” alisisitiza mhandisi Shauri.

Amesema wakati ujenzi ukiwa unaendelea vyema daladala zingeendelea kupita/kutumia barabara za pembeni (access roads) badala ya kutumia barabara kubwa kwani itapunguza sana msongamano.

“Katika kipindi hiki usimamiaji wa zoezi hili linahitaji kuungwa mkono na askari wa barabarani ilikuwadhibiti madereva wote wanatembea kwa mwendo kasi ilikupunguza ajali ambazo zinaweza kuepukika.

Kwa mujibu wa mhandisi Shauri, vituo vya kudumu vya kugeuzia (permanent U-turns) vitajengwa Kimara Baruti, Kimara Butcher na Kimara Mwisho.

Mradi huo mkubwa wa ujenzi unasimamiwa na Wakala wa Usimamizi wa Barabara nchini (TANROADS). DART ipo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).

Hivi karibu waziri wa Ujenzi, Dkt. John Magufuli alifanya ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa barabara ya  mradi wa mabasi yaendayo haraka ambapo alilidhishwa na maendeleo ya ujenzi unaofanywa na kampuni ya STRABAG kutoka ujerumani.


Mwisho.

No comments: