Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Wadau wanaoshughulika moja kwa moja na mchakato wa usajili wa
makampuni hapa nchini wametakiwa kufanya kazi kwa karibu zaidi ili kuimarisha
kiwango cha Tanzania kimataifa katika kujenga mazingira ya biashara.
Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Dk. Florens Turuka amewaambia
waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam wakati wa mkutano wa CEO
Roundtable kuwa mamlaka hizo zinatakiwa kutekeleza mradi unaojulikana kama Tanzania Investment Window Project kabla ya
mwezi Mei mwaka huu ili faida za ubunifu wake ziweze kuunganishwa katika
viwango vya mwaka kesho vinavyohusiana na jinsi nchi zinavyoimarisha mazingira
ya biashara.
Mradi huo unaofadhiliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo
(UNDP) na mpango wa ONE UN, unalenga kuwezesha makampuni ya ndani na ya nje
kujisajili kwa urahisi zaidi na kwa muda mfupi.
Kituo cha Uwekezaji nchini (TIC) kwa msaada wa kiufundi toka shirika
la umoja wa mataifa linalohusika na biashara na maendeleo (UNCTAD) kiko katika
juhudi kuhakikisha kuwa taratibu za usajili wa makampuni unarahisishwa kupitia
mtandao.
Mpango huo
uliasisiwa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda mwezi wa Kumi mwaka jana nchini China.
Mpango huo
utaruhusu wawekezaji kusajili makampuni, kupata vibali vya uwekezaji, vibali
vya kazi na huduma nyingine kupitia njia ya mtandao.
Dk. Turuka
alitaja baadhi ya taasisi zinazotakiwa kufanya kazi kwa karibu kama Wakala wa
Usajili wa Makampuni (Brela), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Wizara ya
Biashara, Mamlaka ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (SSRA), Jiji la Dar es Salaam
na TIC.
“Mamlaka hizi ziteue wawakilishi wa ngazi za
juu kabisa watakaofuatilia kwa haraka utekelezaji wa mradi huu,” alisema, huku
akipendekeza kikosi kazi hicho kukutana kila mwezi kuhakikisha kila kitu
kinakwenda sawa.
Alisema kuwa
mradi huo unachukuliwa kwa umakini mkubwa na Waziri Mkuu Pinda ambaye ametaka
kuelezwa kila wakati maendeleo yake hadi pale utakapotekelezwa.
Pia alitoa
shukrani zake kwa wadau wote waliowezesha mradi kufikia hatua iliyofikiwa hadi
sasa kwa kipindi cha mwaka uliopita hasa kuhusiana na taarifa zinazohusu
taratibu za uwekezaji.
Alisema hadi
sasa taratibu 30 ziko wazi na zinaweza kufikiwa kirahisi kupitia mtandao wa TIC
katika lugha zaidi ya 70.
Alisema taarifa
hizo zinazopatikana kwa sasa zimeonyesha mafanikio makubwa kwa kuwa sasa kila
wiki zaidi ya wafanyabiashara 1000 duniani kote wanatembelea mtandao huo na
idadi ikiongezeka.
Akifafanua
zaidi alisema sekta binafsi inataka kurahisishiwa mambo na kuwa hilo katika
dunia ya leo linaweza kufanikishwa kwa kutumia mtandao.
“Mradi huu
unaweza kufanikisha malengo hayo,” alisema.
Mwisho
No comments:
Post a Comment